• HABARI MPYA

    Monday, February 18, 2013

    WANARIADHA NYOTA TANZANIA WATHIBITISHA KUSHIRIKI KILI MARATHON

    Wanariadha walioshiriki Mili Marathon mwaka jana

    Na Princess Asia
    WANARIADHA mashuhuri wa Tanzania wamethibitisha kushiriki kwenye mbio za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika tarehe 3 Machi 2013 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
    John Bayo, Mkurugenzi wa Mbio za Kilimanjaro Marathon alisema katika taarifa yake jana kwamba wanariadha maarufu Watanzania ambao wameshiriki na kushinda mashindano mbalimbali duniani ikiwemo Kilimanjaro Marathon watashiriki katika mbio hizo kubwa zaidi hapa Tanzania. Baadhi yao ni pamoja na Patrick Nyangero, Andrea Silvini, Fabian Joseph, Sarah Ramadhan, Mary Naali na Banualie Brighton.
    Patrick Nyangero alishika nafasi ya pili kwenye Kilimanjaro Marathon mwaka 2009 ambapo alimaliza mbio katika muda wa 02:15:35, ameshiriki mashindano mengine mbalimbali yakiwemo Gold Coast Marathon, Mashindano ya Dunia huko Melbourne Australia mwaka 2005, na baadae akashinda Nagpur Marathon huko India. Andrea Silvini alishinda Kilimanjaro Marathon mwaka 2007 na baada ya hapo akashinda Pune Marathon mwaka 2008 na akawa mshindi wa tatu kwenye Kilimanjaro Marathon 2008 ambapo alimaliza mbio katika muda wa 02:16:22. Banuelia Brighton alishinda kilomita 42 kwenye Kilimanjaro Marathon 2008 katika muda wa 02:48:37 na baadae akashinda Kigali Marathon mwaka 2009.
    Wanariadha wengine mashuhuri waliothibitisha ni pamoja na Fabian Joseph ambaye ana rekodi ya kushinda Kilimanjaro Marathon 2010 katika muda wa 1:03:59, ambapo alivunja rekodi ya Mtanzania mwenzake Damian Chopa aliyeshinda mbio hiyo katika muda wa 1:04.43. Damian Chopa pia alishinda Nusu Marathon huko Edmonoton Canada mwaka 2005 katika muda wa 1:01:08.
    Wanariadha wengine waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Mary Naali, mshindi wa Vienna Half Marathon mwaka 2010, Sarah Marja Ramadhan ambaye alimaliza km 42 Kilimanjaro Marathon 2012 katika nafasi ya 11 katika muda wa 2:51.00 ambayo ni rekodi binafsi nzuri zaidi katika miaka mitano.
    Zaidi ya nchi 40 zinatarajiwa kushiriki huku washiriki wan je wakitarajiwa kuwa zaidi ya 600. Washiriki wengi watatokea Afrika Kusini, Uingereza, Zimbabwe, Kenya, New Zealand, China, Canada, Marekani, Australia, France na Italy.
    Washiriki wa mbio hizo watakuwa na uhuru wa kuchagua mbio zipi wakimbie kati ya 42 km Marathon, 21 Half Marathon, GAPCO Disabled Half Marathon na Vodacom 5 Km Fun Run.
    “Kilimanjaro Marathon inatambulika kimataifa ikiwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali. Mbio hizi huvutia wanariadha wa viwango vya juu hivyo kuwapa wanariadha Watanzania nafasi ya kujipima ipasavyo”, alisema John Addison, Mkurugenzi wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon.
    "Uandikishwaji washiriki utafanyika Arusha tarehe 28 February kwenye Hoteli ya New Arusha Hotel na pia tareh 1 na tarehe 2 Machi kwenye hoteli ya Keys mjini Moshi. Hakutakuwa na uandikishwaji wowote utakaofanyika siku ya mbio tarehe 3 Machi 2013. Hata hivyo wanaotaka kujiandikisha mapema wanaweza kufanya hivyo kupitia tovuti ya www.kilimanjaromarathon.com," alisema Addison.
    Mbio hizi zinaratibiwa na Executive Solutions huku wadhamini wakuu wakiwa ni Kilimanjaro Premium Lager. Wadhamini wengine ni GAPCO wanaodhamini Nusu Marathon ya Walemavu na Vodacom wanaodhamini mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run. Wadhamini shirikishi ni pamoja na Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, New Arusha Hotel, Kilimanjaro Water , FastJet na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WANARIADHA NYOTA TANZANIA WATHIBITISHA KUSHIRIKI KILI MARATHON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top