• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 27, 2013

  DIDIER KAVUMBANGU ASHINDWA KUVUNJA REKODI YA MABAO YA BAHANUZI YANGA SC

  Didier Kavumbangu akishangilia bao lake la kwanza kufunga mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, dhidi ya African Lyon kwa penalti
  Na Mahmoud Zubeiry
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu tayari amecheza mechi mbili zaidi ya mzalendo, Said Bahanuzi, lakini bado hajafikia idadi ya mabao ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.
  Kavumbangu aliyesajiliwa msimu huu akitokea Atletico Olympique ya Burundi, hadi sasa amecheza 22 na kufunga mabao 10, moja kwa penalti.
  Kavumbangu, ambaye mabao nane kati ya hayo amefunga Ligi Kuu, saba mzunguko wa kwanza na moja mzunguko wa pili, awali kwa kasi aliyoanza nayo alitarajiwa kumpiku haraka Bahanuzi, lakini imekuwa tofauti.
  Bahanuzi alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Yanga, wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka jana haadi akaiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe, yeye akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake saba.
  Hata hivyo, mwanzoni mwa Ligi Kuu aliumia nyama za paja na kukaa nje kwa muda mrefu kabla ya kurudi uwanjani siku za karibuni, tena muda mrefu akianzia benchi.
  Hadi sasa, Bahanuzi ameichezea Yanga katika mechi 20 na kufunga mabao 13, matatu kwa penalti.
  Katika wachezaji wengine wapya Yanga, Simon Masuva amefunga mabao matano katika mechi 22, Nizar Khalfan ambaye mara nyingi hutokea benchi kati ya mara chache (13) alizocheza, amemudu kufunga mabao manne na beki Mbuyu Twite amefunga mabao matatu katika mechi 18.
  Wachezaji wote hao leo watakuwa na nafasi ya kutanua akaunti zao mabao Yanga, iwapo watapangwa katika mechi dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa marudiano baina ya timu hizo, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

  REKODI YA WACHEZAJI WAPYA YANGA SC:
  MCHEZAJI MABAO MECHI
  Said Bahanuzi Yanga 13 20 3penalti
  D. Kavumbangu Yanga 10 22 1penalti
  Simon Msuva Yanga 5 22
  Nizar Khalfan Yanga 4 13
  Mbuyu Twite Yanga 3 18
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DIDIER KAVUMBANGU ASHINDWA KUVUNJA REKODI YA MABAO YA BAHANUZI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top