• HABARI MPYA

  Wednesday, February 20, 2013

  HILI NI DOA CHAFU KWENYE SOKA YETU, HADI FIFA?

  Na Bin Zubeiry

  SAKATA la Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limechukua sura mpya baada ya jana rais wa shiriksiho hilo, Leodegar Chillah Tenga kusema, FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) litatuma wawakilishi wake mwezi ujao nchini kuja kutazama suala la mgombea Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya shirikisho hilo.
  Hatua hiyo inafuatia Malinzi kupeleka malalamiko yake FIFA, baada ya kujiridhisha hatendewi haki katika mchakato mzima wa uchaguzi huo.
  Malinzi aliomba kwa mara ya pili mfululizo kugombea urais wa TFF, baada ya awali mwaka 2008, kugombea na kushindwa na Tenga.
  Baada ya kuchukua fomu na kurejesha, aliwekewa pingamizi na mtu aliyetambulishwa kama Agape Fuwe ambaye hata hivyo, siku ya usikilizwaji wa pingamizi hakutokea.
  Malinzi akavuka kikwazo hicho cha pingamizi, lakini ajabu suala la Fuwe likahamishiwa Kamati ya Rufaa, ingawa halikufanyiwa kazi katika Kamati ya Uchaguzi.
  Kila mara, Tenga anasistiza juu ya kufuatwa kwa utaratibu, kuheshimiwa kwa Katiba na kanuni katika masuala mbalimbali kwenye soka yetu, lakini ukilitazama hili la pingamizi la Fuwe halikuwa ndani ya utaratibu.
  Hilo moja, lakini pili hata sababu ambazo zinaifanya Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kumuengua Malinzi, katika mtazamo wa kawaida sana, halimshawishi mtu yeyote kukubali mgombea huyu anatendewa haki.
  Malinzi aligombea mwaka 2008 chini ya utaratibu kama huu wa leo, sasa iweje leo aambiwe hana sifa? Na ukienda kwenye uhalisia, si kweli Malinzi hana uzoefu? Hapana, ana uzoefu wa kutosha kukidhi matakwa ya kipengele hicho cha kanuni ndani ya Katiba ya TFF.
  Na kwa sababu ya kuamini hatendewi haki, ndiyo maana sasa Malinzi anaamua kupiga hatua zaidi katika kutafuta haki yake. Hakuna ubishi, hapa Malinzi anatafuta haki yake.
  Wasiwasi wangu mkubwa ni mmoja tu; Kitendo cha kushindwa kutatua matatizo yetu wenyewe, hadi tunatumiwa watu waje kutusuluhisha ni aibu na fedheha kwa soka yetu.
  Tunaonekana tuna matatizo makubwa. Dunia itajua hivyo, kwamba Tanzania wana mgogoro ambao FIFA imeingilia kuja kutatua.
  Lakini ni mgogoro wa aina gani ambao tumeshindwa kuutatua wenyewe? Hilo ndilo swali. 
  Watanzania wote hatujui kama Malinzi ana au hana uzoefu wa kutosha kukidhi matakwa ya kanuni ya uchaguzi ya TFF hadi FIFA waje kulitazama hilo? Hapana.
  Katika makala yangu iliyopita, nilisema wazi kuna watu wanatengenezewa mazingira ya kushinda kwa urahisi uchaguzi huu, na unaweza kujionea hii ndiyo sababu Malinzi anaenguliwa.
  Mgongano wa kimaslahi ndani ya Kamati ya Rufaa, kitu ambacho kinaonekana wazi, kinaweza kuwa chanzo cha matatizo yote haya.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, Iddi Mtiginjola ni swahiba wa mgombea pekee wa urais aliyepitishwa, Athumani Jumanne Nyamlani na anaonekana kutaka kumbeba jamaa yake kwa kumuepushia upinzani wa Malinzi.
  Lakini wakati yanafanyika yote haya, watu wanaangalia upande wa pili athari zake ni zipi? Achana na hilo la kujitia doa kimataifa, lakini hata kwa hapa nyumbani, tunawapa ujumbe gani watu?
  Katika siku za karibuni tumeshuhudia taasisi, watu binafsi na makampuni yakijivuta kusaidia soka, kwa sababu ya imani iliyojengeka kwamba sasa mchezo huo umestaarabika.
  Lakini leo, wengine wamekwenda FIFA, wengine wamekwenda mahakamani, wengine wanakandia kwenye vyombo vya habari, hii ni picha gani?
  Kweli tumeshindwa wenyewe kutatua tatizo hili la Malinzi hadi, inafikia FIFA wanakuja kutusaidia? Ni aibu kwa kweli! Siku njema.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HILI NI DOA CHAFU KWENYE SOKA YETU, HADI FIFA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top