• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 27, 2013

  MTIBWA WAMESAHAU SIRI YA MAFANIKIO YAO, AU BIASHARA NDIYO IMEWANOGEA?

  Na Bin Zubeiry
  MTIBWA Sugar ya Morogoro ni timu pekee nje ya Simba SC na Yanga, iliyoweza kutwaa zaidi ya mara moja ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara, mwaka 1999 na 2000 wakati huo Ligi Kuu, ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager.
  Cosmopolitan ya Dar es Salaam ilikuwa timu ya pili mwaka 1967 kuchukua ubingwa wa Bara, baada ya Sunderland (sasa Simba SC) kutwaa taji hilo 1965 na 1966, ingawa wakati wote huo zilikuwa zikishiriki timu za Dar es Salaam pekee.
  Rasmi Ligi ya nchi nzima ilikuja mwaka 1968 na Yanga ikawa bingwa wa kwanza na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kucheza michuano ya Afrika, Klabu Bingwa Afrika ambako ilifika Robo Fainali mwaka 1969 na kutolewa na Asanye Kotoko ya Ghana.
  Zaidi ya Cosmo, timu nyingine zilizochukua ubingwa wa Bara ni Mseto ya Morogoro mwaka 1975, Pan African ya Dar es Salaam mwaka 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya mwaka 1986 na Coastal Union ya Tanga mwaka 1988, zote mara moja moja.
  Mtibwa iliweza kuwa bingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 1999, ikiwa ni mwaka wa tatu tangu ipande ligi hiyo kwa mara ya kwanza kabisa, mwaka 1996.
  Siri ya mafanikio yake ni uwekezaji wa wamiliki wake, kampuni ya Superdoll, ambao walipambana na vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga SC katika kusajili wachezaji bora.
  Ilifanya usajili wa kishindo mwaka 1999, ikichukua nyota kama Monja Liseki, Alphonce Modest, Mtwa Kihwelo waliokuwa Yanga SC, Duwa Said na Steven Nemes kutoka Simba SC na wengine waliokuwa waking’ara timu ya taifa, kama John Thomas Masamaki (marehemu) na Geoffrey Kikumbizi.
  Hiyo ndiyo siri ya mafanikio ya Mtibwa  wakati huo na baada ya hapo, misingi imara ya uwekezaji ndani ya timu hiyo ikaendelea, hadi ikawa inatoa upinzani mkubwa kwa Simba na Yanga katika kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Afrika.
  Prisons iliibuka kuwa timu nyingine pinzani katika nafasi za kucheza michuano ya Afrika, lakini haikuwahi kubeba ubingwa wa Bara.
  Lakini ghafla makali ya Mtibwa yakaanza kupotea, na kubaki kuwa timu ya kucheza Ligi Kuu ili ibaki na si washindani tena, jambo ambalo kwa kiasi fulani liliathiri msisimko wa soka ya nchi hii, kwa sababu ilibaki kuwa ligi ya Simba na Yanga.
  Mungu saidia ujio wa Azam Ligi Kuu mwaka 2008, hatimaye leo Simba na Yanga zimepata mpinzani wa kweli katika mbio za ubingwa.
  Siri ya mafanikio ya Azam ni ile ile kama ya Mtibwa, uwekezaji. Azam wamewekeza, kwa kusajili wachezaji wazuri na walimu bora, ambao matokeo yake ni kuwa na timu nzuri ya ushindani.
  Lakini Ligi Kuu ya timu tatu tu haitoshi, tunahitaji kuwa na Ligi Kuu ya timu imara angalau tano, ambazo zote moja kati yao inaweza kuchukua ubingwa.
  Timu za majeshi pamoja na wachezaji wake kuwa na huduma nzuri na za uhakika, zimepoteza mwelekeo kutokana na kile kinachoonekana wazi kukosa viongozi bora.
  Timu za makampuni kama Mtibwa na Kagera Sugar nazo zinaelekea kutosheka na uhakika wa kucheza Ligi Kuu pekee na si zaidi ya hapo.
  Mtibwa imetuonyesha mfano msimu huu, kwa kujikusanyia pointi 10 kutoka kwa Simba na Yanga kati ya pointi zao 27 walizovuna katika mechi 18 walizocheza hadi sasa.
  Dhahiri uimara huu wa Mtibwa umetokana na timu nzuri waliyonayo kwa sasa, maandalizi mazuri na dhamira ya kushindana.
  Yapo mambo mawili matatu yaliyoishusha Mtibwa, kubwa ni sera kama za Arsene Wenger pale Arsenal ya England, kuuza wachezaji wake nyota kila msimu.
  Hii imekuwa ikiwarudisha nyuma Mtibwa kila msimu- subiri mwishoni mwa msimu, kuna wachezaji kama Issa Rashid, Salvatory Ntebe na Hussein Javu wanaweza kuuzwa.
  Huwezi kuizuia timu kuuza mchezaji, huo ndio mfumo wa soka ya kulipwa, lakini wakati mwingine timu inaweza kujiwekea sera kwa ajili ya kutimiza malengo yake na tumeshuhudia timu zikigoma kuuza wachezaji wake, hata Ulaya.
  Hata Mtibwa wanatakiwa kuangalia mara mbili sera yao ya kuuza uza wachezaji wao nyota kila msimu, kama itaweza kuwarudishia matunda waliyovuna 1999 na 2000, heshima ambayo hadi hii leo haijafikiwa na timu nyingine nje ya Simba na Yanga.
  Nimekumbushia siri ya mafanikio ya timu hiyo katika siku zake za mwanzoni Ligi Kuu, kwamba ni uwekezaji katika timu- na uzuri Mtibwa ni timu ambayo wamiliki wake wana uwezo, hata usiwe kama wa Azam, lakini wanaweza kuhudumia vema timu yao.
  Tunazungumzia maslahi ya soka ya Tanzania, hatuwezi kuwa na timu bora za taifa, bila kuwa ni klabu madhubuti na ligi ya ushindani.
  Azam kwa sasa ndiyo timu inayoshindana na Simba na Yanga katika Ligi Kuu, lakini msimu huu hadi sasa haijavuna hata pointi moja kwa timu hizo, ila Mtibwa imevuna pointi 10, maana yake inaweza kushindana nazo, nayo ikatengeneza orodha ya timu nne tishio katika Ligi Kuu.
  Ni hadi hapo watakapoamua wenyewe Mtibwa Sugar, kusuka au kunyoa. Ila, msimu huu wametuonyesha wanaweza wakiamua. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MTIBWA WAMESAHAU SIRI YA MAFANIKIO YAO, AU BIASHARA NDIYO IMEWANOGEA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top