• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 23, 2013

  BRANDTS: AZAM WAZURI LAKINI SIYO KWETU, SISI TUNATISHA CECAFA NZIMA

  Brandts; Azam wazuri, lakini si kwetu, sisi wabaya

  Na Mahmoud Zubeiry
  KOCHA wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amesema kwamba Azam FC ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri, lakini haiwezi kuwazuia leo kuchukua pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Bagamoyo jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto amesema kwamba kocha wao anajiamini anashinda mechi ya leo.
  Kizuguto amesema kwamba Brandts aliishuhudia Azam FC ikiilaza JKT Ruvu mabao 4-0 katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na amekiri ni timu nzuri, lakini amesema haiwatishi.
  “Amesema Azam hawamtishi, kwa sababu Yanga ni timu bora kuliko zote Afrika Mashariki na Kati kwa sasa na atawafunga,”alisema Kizuguto akimnukuu beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi.
  Aidha, Kuzuguto amesema Brandts akiizungumzia ligi kwa ujumla, amesema ni ngumu na kila timu inataka kushinda na kwamba Yanga inakumbana na upinzani huo na inakabiliana nao. 
  “Amesema wanapambana, ligi ni ngumu, timu nyingine wanazizidi uwezo, lakini wanakosa bahati ya kushinda kama mechi na Mtibwa (Sugar), tulitoa sare (ya 1-1), lakini tulipoteza nafasi nyingi za kufunga,”amesema Kizuguto.
  Hata hivyo, Ofisa huyo amesema kwamba, kocha wao huyo anajivunia kitu kimoja, kwamba tayari amekwishazizoea timu za Tanzania, hivyo Azam hawamnyimi raha kabisa.
  Yanga ilikuwa imeweka kambi katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo tangu mwanzoni mwa wiki na inatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam kuingia uwanjani kumenyana na washindani wao hao wakuu katika mbio za ubingwa.
  Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa wastani wake mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa inalingana kwa pointi na Azam FC, 36 kila moja, ingawa Wana Lamba Lamba wamecheza mechi moja zaidi.
  Huo utakuwa mchezo wa 19 kwa Brandts kuiongoza Yanga, tangu arithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet Septemba mwaka huu.
  Katika mechi 18 za awali, Brandts ameiwezesha Yanga kushinda  mechi 11, kufungwa nne na sare tatu.

  REKODI YA ERNIE BRANDTS YANGA
  Yanga 1-1 Simba SC (Ligi Kuu) 
  Yanga 0-1 Kagera Sugar         (Ligi Kuu)
  Yanga 3-1 Toto African         (Ligi Kuu)
  Yanga 3-2 Ruvu Shooting         (Ligi Kuu)
  Yanga 3-0 Polisi Moro (Ligi Kuu)
  Yanga 1-0 JKT Oljoro (Ligi Kuu)
  Yanga 3-0 JKT Mgambo         (Ligi Kuu) 
  Yanga 2-0 Azam FC (Ligi Kuu)
  Yanga 2-0 Coastal (Ligi Kuu)
  Yanga 0-1 Tusker (Kirafiki) 
  Yanga 1-1 Ariminia Bielefed      (Kirafiki)
  Yanga SC 0-2 Emmen FC (Kirafiki)
  Yanga SC 1-2 Denizlispor FC   (Kirafiki)
  Yanga SC 3-2 Black Leopard    (Kirafiki)
  Yanga SC 2-1 Black Leopard    (Kirafiki) 
  Yanga SC 3-1 Prisons               (Ligi Kuu)
  Yanga 1-1 Mtibwa Sugar           (Ligi Kuu)
  Yanga 4-0 African Lyon             (Ligi Kuu)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BRANDTS: AZAM WAZURI LAKINI SIYO KWETU, SISI TUNATISHA CECAFA NZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top