• HABARI MPYA

    Friday, February 22, 2013

    MILOVAN KAIHARIBU SANA SIMBA SC, ASEMA HANS POPPE


    Kapteni wa zamani JWTZ, Zacharia Hans Poppe: Milovan katuharibia sana Simba yetu

    Na Mahmoud Zubeiry
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe, amesema kwamba waliamua kuachana na kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick baada ya kugundua ‘hana jipya’ na anazidi kuwaharibia timu.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana kwa simu kutoka Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasika ya Kongo (DRC), Hans Poppe alisema kwamba Milovan ndiye ameiporomosha Simba SC kutoka kuwa bingwa hadi kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba kocha huyo pamoja na udhaifu wote alionao kiutendaji, lakini pia alikuwa hashauriki, kiasi cha kuitia hasara kubwa klabu.
    Milovan; Hasara tupu na Simba hawana hamu naye
    Hans Poppe alisema anashangazwa na wapenzi wa Simba kumshangilia hivi sasa Milovan wanapomuona Uwanja wa Taifa, wakati wenyewe ndio waliotaka kumpiga baada ya Simba kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mjini Morogoro.   
    “Walitaka kumpiga na mimi ndiye niliyemsaidia, nilimvuta na kukaa naye karibu yangu nikiwasihi wasimpige, ndipo wakaacha, sasa leo wao hao hao wanamshangilia kana kwamba aliifanyia jambo la maana sana Simba SC, kumbe katuharibia timu tu,”alisema Hans Poppe.
    Mwenyekiti huyo alisema kwamba umefika wakati sasa lazima wapenzi wa soka nchi hii waangalia kitu kinachofanywa na makocha katika timu, badala ya kuwababaikia bila sababu yoyote, akimtolea mfano Milovan kwamba alikuwa anapewa fedha nyingi, lakini hakuna cha maana alichoifanyia klabu.
    “Yule bwana mimi mwenyewe nilishamfuatilia sana na kugundua hana lolote, siku moja kwenye mechi na Azam ile tuliyoshinda 3-2, wakati wa mapumziko nilimfuatilia chumba cha kubadilishia nguo wakati huo timu iko nyuma.
    “Nilipofika sikumkuta, alikuwa anavuta sigara chooni, sasa kaja baadaye kafikia kula ndizi, baada ya hapo akawaambia wachezaji, msiwe na wasiwasi hii mechi tunashinda, nendeni mkajitume, basi,”alisema.
    Hans Poppe alisema alistaajabishwa mno na kitendo cha kocha huyo, kwani alitarajia angewaambia wachezaji mapungufu yao katika dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuwapa mbinu mpya za kwenda kutafuta ushindi kipindi cha pili, lakini hakufanya hivyo.
    Hans Poppe amesema Milovan aliikuta Simba ikiwa timu nzuri, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na makocha waliomtangulia kuanzia Patrick Phiri wa Zambia na Moses Basena wa Uganda, lakini yeye akaibomoa taratibu.
    Hans Poppe amesema Milovan pia amechangia kwa kiasi kikubwa kushusha nidhamu ya wachezaji wa Simba kutokana na tabia yake yeye mwenyewe binafsi kutokuwa mfano mzuri. “Yapo mambo ambayo hatuwezi kusema hadharani,”. 
    “Hadi sasa imefikia huyu kocha wa sasa ana mzigo mkubwa. Milovan alikuwa hasikilizi ushauri wa mtu na hakuwa mtendaji mzuri, uongozi ulikuwa sahihi kumfukuza, na sikufichi, mimi inaniuma sana, kwa hasara aliyoitia Simba, halafu ananondoka analipwa fedha zake,”alisema Hans Poppe.
    Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi mwaka 2008, Milovan alirejeshwa Simba SC Januari mwaka jana na kuiongoza timu katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, akirithi mikoba ya Basena, ambaye alifukuzwa akiiacha timu inaongoza Ligi Kuu.
    Milovan alimalizia vema msimu katika Ligi Kuu, akiiwezesha Simba SC kuchukua ubingwa, ikiwafunga wapinzani wa jadi, Yanga SC mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho.
    Lakini baada ya hapo, Simba imekuwa ikifululiza kufanya vibaya kuanzia kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu pia hadi mwishoni mwa mzunguko wa kwanza alipotupiwa virago.    
    Kwa sasa, Simba SC ipo chini ya Kocha Mfaransa, Patrick Liewig anayesaidiwa na Basena na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’. 

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MILOVAN KAIHARIBU SANA SIMBA SC, ASEMA HANS POPPE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top