• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 25, 2013

  YANGA WAINGIA KAMBINI HOTELI YA TAIFA STARS KUJIANDAA NA MECHI NA KAGERA SUGAR

  Baadhi ya wachezaji wa Yanga, Haruna Niyonzima kulia, Nadir Haroub 'Cannavaro, Oscar Joshuia na Athumani Iddi 'Chuji', aliyeipa mgongo kamera katika mechi dhidi ya Azam waliyoshinda 1-0 na kuzidi kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu. Leo wameingia kambini Tansoma.
  Na Baraka Kizuguto
  BAADA ya kuichapa Azam FC kwa bao 1-0 mwishoni mwa wiki, timu ya Yanga leo imeingia kambini katika Hoteli ya Tansoma katikati ya jiji, kujiaandaa na mechi inayofuata dhidi ya timu ya Kagera Sugar, mchezo utakaofanyika keshokutwa Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 jioni.
  Tansoma ndiyo sehemu ambayo timu ya taifa, Taifa Stars imekuwa kambi katika siku za karibuni.
  Yanga, ambayo iliwapa furaha washabiki, wapenzi wa soka na wanachama wake kwa soka safi la ufundi wa hali ya juu, itashuka dimbani kuwakabili wakata miwa hao ambao katika mchezo wa awal waliibuka na ushindi wa bao 1-0 mchezo uliofanyika katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba.
  Yanga, yenye jumla ya point 39 na mabao 34 ya kufunga na mabao 12 ya kufungwa itashuka Uwanja wa Taifa kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo ili kuendelea kuongoza  msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hatimaye iweze kutwaa ubingwa.
  Mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts amesema anashukuru vijana wake kwa kufanya kile alichowaagiza, nidhamu ya hali ya juu na kushika maelekezo yake ndio vitu vilivyopelekea kuendelea kuibuka na ushindi katika michezo mbali mbali waliyocheza.
  “Nawapongeza washabiki, wanachama na wapenzi wa Yanga waliojitokeza kwa wingi siku ya jumamosi, kuja kuwashangilia vijana, kikubwa nawaomba waendelee na moyo huo huo, kwani waliwapa nguvu vijana na kuwafanya wacheze kwa kujiamini mda wote wa mchezo,”alisema Brandts.
  Aidha, Brandts alisema matokeo ya juzi yameendelea kuiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kuelekea kutwaa Ubingwa na atahakikisha wanajitahidi kushinda kila mchezo ili kujiweka katika mazingia mazuri ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom.
  Kikosi cha  wachezaji 26 na benchi la ufundi wote wameingia kambini katika Hoteli ya Tansoma mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi na wachezaji wote ni wazima kiafya na kiakili hivyo hakuna mcheaji hata mmoja ambaye ni majeruhi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA WAINGIA KAMBINI HOTELI YA TAIFA STARS KUJIANDAA NA MECHI NA KAGERA SUGAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top