• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 19, 2013

  YANGA SC: AZAM NA SISI NDIO FAINALI YA UBINGWA JUMAMOSI

  Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts (kushoto) akiwanoa vijana wake

  Na Mahmoud Zubeiry
  YANGA SC imesema mechi kati yao na Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ndiyo fainali ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Msemaji wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, uongozi wa klabu hiyo na benchi la ufundi kwa ujumla pamoja na wachezaji, wanaipa uzito mkubwa mechi hiyo.
  “Mechi hii inapewa uzito mkubwa sana. Ni mechi ambayo lazima tushinde ili kuweka vizuri mazingira ya ubingwa, kwa sababu Azam ndio wapinzani wetu katika  mbio hizi,”alisema Kizuguto.
  Ofisa huyo amesema timu inaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo huo, ikiwa inajifua kwenye Uwanja wa Mabatini, Kijitonyama, Dar es Salaam.
  Amesema hakuna majeruhi hata mmoja kwenye kikosi chao na wachezaji wana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo.
  Kizuguto amesema timu itaingia kambini kuanzia Jumatano kufanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mechi hiyo, inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua. 
  Kwa sasa, Yanga SC ndio inaongoza Ligi Kuu ya Vodacom ikiwa na pointi 36, baada ya kucheza mechi 16, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 33.
  Hali ni mbaya kwa mabingwa watetezi, Simba SC wanaoshika nafasi ya tatu kwa pointi zao 28 hadi sasa, ingawa wamecheza mechi sawa na Yanga na Azam, 16.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA SC: AZAM NA SISI NDIO FAINALI YA UBINGWA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top