• HABARI MPYA

    Saturday, February 16, 2013

    AZAM YAANZA VYEMA AFRIKA

    Kipre Tchetche; Shujaa wa Aza leo

    Na Mahmoud Zubeiry
    AZAM imeanza vyema safari yake mashindano ya Afrika, baada ya kuilaza Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, mabao 3-1 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Shukrani kwake mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliyefunga mabao mawili ndani ya 10 dakika za mwisho na kuipa ushindi timu hiyo ya Chamazi. 
    Kwa matokeo hayo, Azam sasa inahitaji sare tu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Sudan Kusini, au kufungwa si kwa zadi ya tofauti ya bao moja ili kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Azam wakitangulia kufunga bao kupitia kwa Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 14, kabla ya Al Nasir kusawazisha kupitia kwa Fabian Elias dakika ya 38.
    Babbi alifunga bao lake akiunganisha krosi ya kiungo Mkenya, Humphrey Mieno wakati bao la Nasir lilitokana na shambulizi la kushitukiza, Azam wakitoka kushambulia.
    Wachezaji wa Azam wakimpongeza Babbi kufunga bao la kwanza leo
    Refa David Omweno, aliyesaidiwa na Peter Keireini na Gilbert Cheruiyot wote wa Kenya, walishindwa kuwadhibiti wachezaji wa Nasir waliocheza rafu za hatari, kiasi cha kuwaumiza wachezaji wawili wa Azam walioshindwa kumalizia japo dakika 45 za kipindi cha kwanza.
    Hao ni kiungo kutoka Ivory Coast, Kipre Michael Balou na mshambuliaji kutoka Uganda, Brian Umony.
    Kipindi cha pili kwa Azam kilianza kwa ugumu kidogo, timu zote zikishambuliana kwa zamu na kuonekana kama mchezo utamalizika kwa sare au timu yoyote kushinda.
    Hata hivyo, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Muingereza, Stewart Hall kumtoa mfungaji wa bao la kwanza, Babbi na kumuingiza mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ yaliibeba Azam.
    Adebayor aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu Desemba mwanzoni mwaka jana, alikwenda kubadilisha kabisa sura ya mchezo, akiichachafya mno ngome ya Nasir.
    Presha ya Adebayor iliisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa mabao ya ushindi ya Azam.
    Azam ilipata bao lake la pili dakika ya 80, mfungaji Kipre Tchetche akiunganisha krosi ya Khamis Mcha ‘Vialli’.
    Wakati mashabiki wanaaachia siti zao, Kipre Tchetche tena aliwainua vitini mashabiki kwa kuifungia bao la pili Azam akimalizia pasi nzuri ya Mieno.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Himid Mao, David Mwantika, Jockins Atudo, Kipre Balou/Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, Humphrey Mieno, Abdi Kassim/John Bocco na Brian Umony/Khamis Mcha ‘Vialli’.
    Al Nasir; Peter Midia, Joseph Odongi, Miskin Emmanuel, Abdalah Sebit, Simon Amanya, Johnson James/Adova Nam, Abdulmalik Sebit/Emmanuel Manas, Ladu Manas, Kon James, Jacob Osuru na Fabian Elias.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM YAANZA VYEMA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top