• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 21, 2013

  MALKIA WA NYUKI AWATUPIA VIRAGO BABU MFARANSA NA BASENA SIMBA SC, AMKABIDHI TIMU JULIO

  Malkia wa Nyuki, Rahma Al Kharoos akizungumza jana

  Na Mahmoud Zubeiry
  MFADHILI wa Simba SC, Rahma Al Kharoos amesema kwamba timu hiyo kwa sasa haistahili kufundishwa na kocha kutoka nje, kwa sababu haina wachezaji wataalamu na wenye ubora na viwango, hivyo amependekeza iwe chini ya mzalendo Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ pekee. 
  Akizungumza na Waandishi wa Habari jana katika hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam, Rahma maarufu kama Malkia wa Nyuki, amesema kwamba kama Simba wanataka kuwa na makocha wa kigeni, basi watafute wachezaji wataalamu na wenye ubora na viwango. 
  “Unajua ukikaa ukiangalia timu inavyoendelea ya Simba, tofauti na uwezo wake na kocha kutoka nje, sawa sawa na mtoto wa shule ya vidudu, unampa mwalimu wa chuo kikuu. Kwani sisi hatuna makocha hapa, si tuna makocha,”alisema.
  Aidha, Mama Salma ambaye jana aliahidi kumlipa malimbikizo yake ya mishahara ya miezi mitatu kocha aliyetupiwa virago Simba SC, Mseriba Profesa Milovan Cirkovick (dola za kimarekani 24,000), alisikitikia makocha wa kigeni kupewa fedha nyingi, wakati wazawa wapo na wana uwezo.
   “Fedha hizi dola 8,000 (kwa mwezi) anayopewa (Milovan), makocha wangapi watafaidika hapa, sasa hivi hii fedha inakweenda nje, faida yake nini, kwa nini wasipewe makocha wazawa, wampe hiyo timu Julio,”alisema.
  Mama alisema kwamba hakuna tatizo timu za Tanzania kufundishwa na makocha wazawa, kwa sababu nchi nyingi zinatumia makocha wazawa na akatolea mfano Oman kwamba timu nyingi zinatumia makocha wa Tanzania.
  “Kwa nini sisi tutafute makocha wa nje halafu hatuwezi kuwalipa, kwa sababu gani, kwa sababu ya sifa, haiko hivyo, sasa hivi lazima tubadilike. Mkwasa (Charles Boniface) alikuwa anafundisha Twiga Stars, timu ya wanawake, timu ngumu zaidi, lakini ameifundisha na kaifikisha hapo ilipo.
  Huyo Julio si alikuwa Oman, si alikuwa anafundisha timu nzuri Oman, sasa tatizo liko wapi, tatizo tuwape fursa wenzetu hapa, kama mnataka kuleta makocha wa nje, tafuteni na wachezaji wataalamu, ambao watakuwa wapo kwenye ubora na  viwango,”alisema Malkia wa Nyuki.
  Kwa sasa, Simba SC inafundishwa na Kocha Mfaransa, Patrick Liewig anayesaidiwa na Mganda, Moses Basena na mzalendo Jamhuri ‘Julio’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MALKIA WA NYUKI AWATUPIA VIRAGO BABU MFARANSA NA BASENA SIMBA SC, AMKABIDHI TIMU JULIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top