• HABARI MPYA

    Tuesday, February 26, 2013

    SIMBA SC WAITISHA MKUTANO MKUU WA DHARULA KUJADILI MWENENDO MBAYA WA TIMU

    Ezekiel Kamwaga akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo Msimbazi, kutangaza Mkutano Mkuu wa dharula

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIKAO cha Kamati ya Utendaji ya Simba SC jana, kimefikia uamuzi wa kuitisha Mkutano Mkuu wa dharula wa klabu hiyo, ambao ajenda yake itakuwa moja tu, kujadili mwenendo wa timu katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba siku na mahali ambako Mkutano huo utafanyika vitatajwa wakati wowote kuanzia sasa.
    Aidha, Kamwaga alisema kwamba hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Simba SC aliyejiuzulu na kwamba uongozi upo pamoja. “Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa klabu ya Simba aliyejiuzulu. Uongozi upo pamoja na mambo yote yatajadiliwa kwenye mkutano huo wa dharula,”alisema.
    Akiuzungumzia mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kamwaga alisema kwamba timu itaondoka Alfajiri ya Ijumaa kwenda Angola kuwavaa wenyeji wao, Recreativo de Libolo.
    Alisema mechi hiyo itafanyika Jumapili mjini Calulo, umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda.
    “Kwa mujibu wa kanuni za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) kama umbali wa mji ambao inachezwa mechi unakuwa ni zaidi ya kilomita 200, timu mwenyeji inatakiwa kumsafirisha mgeni kwa ndege, kwa hivyo ni matumaini yetu, wenyeji wetu watakuwa tayari wametutayarishia ndege, kwa kuwa hatuwezi kusafiri kwa basi kwa zaidi ya saa nne,”alisema Kamwaga.
    Kamwaga alisema kwamba, Mkuu wa msafara wa timu atakuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe, wakati upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utawakilishwa na Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji pia, Muhsin Balhabou.
    Kamwaga alisema kikosi kamili cha Simba kitakachokwenda Angola kitatajwa Alhamisi kwa kuwa leo ni mapema sana, kwani wanahofia anaweza kuumia mchezaji yeyote wakati amekwishatajwa kuwemo kwenye safari.
    Simba SC ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza na Libolo wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ili isonge mbele, inatakiwa kushinda 2-0.
    Mwaka 1978, Simba iliwahi kufanya maajabu ikitoka kufungwa 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia mjini Dar es Salaam katika michuano hiyo hiyo na kwenda kushinda 5-0 ugenini, hivyo kusonga mbele.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC WAITISHA MKUTANO MKUU WA DHARULA KUJADILI MWENENDO MBAYA WA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top