• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 18, 2013

  SIMBA SC BADO INA NAFASI YA KUSONGA MBELE AFRIKA

  Mwinyi Kazimoto kushoto akigombea mpira na kiungo wa Libolo, alikuwa na wakati mgumu sana jana 

  Na Mahmoud Zubeiry
  KIUNGO Amri Kiemba hakuwa katika ubora wake jana. Mwinyi Kazimoto alikuwa na wakati mgumu mbele ya viungo bora wa Recreativo de Libolo ya Angola pamoja na kujitahidi sana.
  Pamoja na hayo, bado safu ya kiungo ya Simba SC ilitengeneza nafasi, japo kwa tabu. Jambo la kusitikisha, pamoja na tabu ya kutengeneza nafasi, lakini mtihani ulikuwa ni jinsi ya kuzitumia.
  Kwa mfumo wowote ule, Simba itafunga kwa urahisi timu dhaifu tu, kwa sababu haina watu ambao unaweza kuwaita washambuliaji. Haruna Moshi ‘Boban’ hayuko katika kiwango kizuri, kwanza- lakini pili hawezi kucheza kama mshambuliaji wa kwanza.
  Na hawezi kabisa kucheza kama mshambuliaji pekee, kwa sababu hana uwezo huo. Soka ya Haruna ni kistaarabu, hawezi purukushani. Mpe mpira kwenye nafasi afanye mambo haraka yawe mambo.
  Sasa taabu ya kumsimamisha mbele ya mabeki wawili- aende nao hewani, agombee nao mipira, huyu si Haruna tuliyemzoea.
  Haruna sana mpange kama mshambuliaji wa pili, acheze na mshambuliaji halisi ambaye atafanya purukushani zote na kumpa mwanya Boban wa kufanya vitu. Hapo utampenda Boban Mawela mtoto wa Mboka Manyema.
  Kuna tatizo moja kwa wachambuzi wetu, mara nyingi wanaangalia matokeo tu na hivi hatuzisaidii timu zetu. Simba SC imefungwa 1-0 nyumbani jana na Recreativo de Libolo ya Angola katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Mrisho Ngassa jana alipambana sana, lakini wapi
  Kwa nini? Kwanza lazima ieleweke mpira ni mchezo wa makosa, lakini pia mpira ni mchezo wa bahati na hayo mawili ndiyo yaliyoiangusha Simba SC jana.
  Walitengeneza nafasi kwa tabu sana, wakashindwa kuzitumia kutokana na udhaifu kwenye safu yao ya ushambuliaji, maana yake bahati haikuwa yao jana. Simba SC walicheza mechi ngumu sana jana na wanakabiliwa na ugumu sana katika mchezo wa marudiano.
  Recreativo ni timu nzuri ya ushindani na inaweza kufika mbali katika michuano ya mwaka huu, kwa sababu hata maandalizi yao ni mazuri. Hii ni timu ambayo unaweza kuona kabisa inakuja kuleta mapinduzi katika soka ya Afrika. Safi sana.
  Kama timu, inacheza kwa mipango, ikipiga pasi za kufika haraka kwenye himaya ya wapinzani na kwa wachezaji mmoja mmoja, wako vizuri sana. 
  Lakini pamoja na nayo, bado Simba ilicheza vizuri jana, walipiga pasi vizuri, walikuwa wanaonana kwa pasi zao za hapa na pale. Kwa wachezaji, waliweza kukabiliana na wachezaji wenye nguvu wa Recreativo. Ilikuwa mechi nzuri.
  Haruna Chanongo akipasua katikati ya mabeki wa Libolo
  Nilimuona Mrisho Ngassa akitumia maarifa na kujituma kutafuta nafasi. Kuna wakati alikuwa akihama upande mmoja hadi mwingine kutafuta nafasi. Yule bwana mdogo Haruna Chanongo kafanya nzuri sana jana, ingawa ilikuwa mechi yake ya kwanza ya kimataifa.
  Simba iliathiriwa na kumkosa Felix Sunzu katika mechi ya jana na mbaya zaidi haina mshambuliaji mbadala, aliopo Abdallah Juma haaminiki.
  Najaribu kukitazama kikosi cha Simba, hadi wachezaji waliopo benchi zaidi ya Sunzu, mshambuliaji ni Abdallah tu, ambaye haaminiki kiasi cha yeye mwenyewe kupoteza kujiamini na hata akipewa nafasi hafanyi vizuri.
  Mashabiki hawamkubali tena, siku akianzishwa wanaanza kumzomea hata kabla hajagusa mpira, ataweza nini?
  Katika mechi kati ya Yanga na African Lyon Ligi Kuu ya Bara, Jerry Tegete alipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga mashabiki wakaanza kumzomea na kupiga kelele atolewe.
  Mwinyi akipambana
  Ilimtoa mchezoni kidogo Tegete, lakini kwa sababu ya uzoefu alionao, alitulia na akafunga mabao mawili katika ushindi wa 4-0 na hakushangilia siku hiyo zaidi ya kupongezana tu na wenzake tena katika hali ya kawaida mno.
  Vivyo hivyo kwa Abdallah, wanapomzomea wanamtoa mchezoni na hawezi kufanya vizuri. Simba wanatakiwa kumpa moyo Abdallah, kumjenga kisaikolojia aweze kucheza, kwa sababu huyu kijana ana uwezo ambao amekwishaudhihirisha katika siku za mwanzoni tu za maisha ya kwenye klabu hiyo.
  Kumponda alifanya nini kwenye mechi iliyopita si jawabu, bali ni vema kutaka kujua kwa nini hafanyi vizuri. Lakini kwa kuwa kuna watu ndani ya Simba wana chuki na yule kijana, basi wanafurahi akiwa katika wakati mgumu, bila kuzingatia maslahi ya timu.
  Kuelekea mchezo wa marudiano, naona kabisa Simba inakabiliwa na mtihani mgumu, lakini unaweza kujipa moyo na kitu kimoja, kwamba katika soka lolote hutokea.
  Nakumbuka, mwaka 1979 Simba ilifungwa 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia Dar es Salaam na watu wakakata tamaa ya timu kusonga mbele, lakini katika mchezo wa marudiano ikashinda 5-0 ugenini na kusonga mbele.    
  Wachezaji wa Simba wakiwapungia mikono mashabiki kabla ya mechi jana
  Mambo kama haya yanawezekana katika soka, ila sasa kunahitajika utulivu ndani ya Simba SC. Kutowachanganya wala kuwavuruga wachezaji na kuhakikisha maandalizi mazuri.
  Kuweka dhamira ya kwenda kupambana kubadilisha matokeo ili timu isonge mbele. Simba wakienda kwenye mchezo wa marudiano wakafanikiwa kupata bao la mapema, watarahisisisha mchezo. Bado Simba ina nafasi, iwapo watafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa jana.
  Mungu asaidie Sunzu apone, lakini hata kama hatapona lazima Simba SC wajipange kwenda kucheza mchezo wa marudiano kwa dhamira ya kushinda na kusonga mbele. Simba bado ina nafasi ya kusonga mbele licha ya kufungwa 1-0 nyumbani jana.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC BADO INA NAFASI YA KUSONGA MBELE AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top