• HABARI MPYA

  Ijumaa, Februari 22, 2013

  ZIMBWE: AZAM ITAZISUMBUA SIMBA NA YANGA, LAKINI HAITAZIPOTEZA

  Omar Zimbwe; Kisiki cha enzi hizo Taifa Stars

  Na Mahmoud Zubeiry
  BEKI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Omar Zimbwe amesema kwamba Simba na Yanga zitaendelea kutawala soka ya Tanzania, kwa sababu zina wapenzi wengi na hiyo ndiyo silaha kuu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY wiki hii, Zimbwe alisema kwamba miongoni mwa wapenzi hao wengi wa Simba na Yanga wapo matajiri na watu wenye mamlaka, ambao wamekuwa wakizisaidia timu hizo.
  Amesema  matatizo kama migogoro hayawezi kufutika moja kwa moja katika klabu hizo, lakini zitaendelea kutawala soka ya Tanzania.
  Zimbwe amekiri Azam FC imeleta changamoto katika soka ya Tanzania, lakini amesema itaendelea kushindana na Simba na Yanga katika kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara.
  “Azam ni timu nzuri, mmiliki wake ni tajiri mkubwa na amewekeza kwenye timu yake, kweli hii timu imeleta changamoto, lakini Simba na Yanga zitaendelea kutamba. 
  Kuna msimu Simba na Yanga zitakaa nafasi mbili za juu, kuna msimu, moja itatoka kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa Yanga na Azam ikaingia, au kama msimu huu Simba inaelekea kuziachia nafasi Yanga na Azam,”alisema.
  Zimbwe amesema muda si mrefu Azam watafuta kiu yao ya kuwania ubingwa wa Bara kwa kutwaa taji na kwamba hata kama isiwe msimu huu, basi misimu michache ijayo kwa sababu timu hiyo imejengwa vizuri.
  “Azam wana timu nzuri, na bado wamiliki wake wanataka kuijenga zaidi iwe nzuri zaidi, kwa hiyo itachukua ubingwa, lakini bado nasistiza Simba na Yanga hazitapotea,”alisema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: ZIMBWE: AZAM ITAZISUMBUA SIMBA NA YANGA, LAKINI HAITAZIPOTEZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top