• HABARI MPYA

  Thursday, April 04, 2019

  WAZIRI MKUU AAGIZA DOSARI ZILIZOJITOKEZA KUFUZU AFCON ZIFANYIWE KAZI TAIFA STARS

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA 
  WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka viongozi, wachezaji na makocha wa Taifa Stars kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita ili kujiweka sawa kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakayofanyika Misri Juni mwaka huu.
  Akiwasilisha hotuba bungeni mjini Dodoma leo kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/20, Majaliwa amewataka wachezaji na viongozi wote wanaohusika na Taifa Stars kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita ili timu hiyo iwe imara zaidi.

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) ameagiza mapungufu yaliyojitokeza Taifa Stars yafanyiwe kazi 

  Amesema timu hiyo inapaswa kwenda Misri kushindana na siyo kushiriki michuano ya Afocn.
  "Itakumbukwa kwamba imepita takriban miaka 39 tangu nchi yetu ishiriki kwa mara ya mwisho michuano ya mpira wa miguu kwa nchi za Bara la Afrika, maarufu Afcon," Waziri Mkuu amesema na kueleza zaidi:
  "Hata hivyo, kusubiri huko kulikoma Machi 24, mwaka huu baada ya vijana wetu wa Taifa Stars kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya jirani zetu wa Uganda. Ushindi huo unaipeleka Taifa Stars katika Afcon 2019 huko Misri.
  "Nitumie fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi, benchi la ufundi, kamati ya uhamasishaji wa ushindi, mashabiki na watanzania wote kwa kutimiza ndoto yetu ya muda mrefu ya kushiriki michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika.
  "Nitoe wito kwa viongozi, wachezaji na walimu kufanyia kazi upungufu uliojitokeza kwenye michezo iliyotangulia ili kujiweka sawa na michuano ya mwezi Juni mwaka huu. Napenda mtambue kwamba lengo letu ni kwenda kushindana na si kushiriki. Niwatakie maandalizi mema na mafanikio katika michuano hiyo inayokuja."
  Taifa Stars imefanikiwa kutinga fainali za michuano hiyo baada ya kuifunga Uganda 3-0 katika mechi yake ya mwisho na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya The Cranes katika kundi ambalo pia lililikuwa na timu za Cape Verde na Lesotho.
  Kabla ya mechi hiyo, Uganda ilikuwa haijaruhu si tu kupoteza mechi, bali pia nyavu zake kutikiswa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI MKUU AAGIZA DOSARI ZILIZOJITOKEZA KUFUZU AFCON ZIFANYIWE KAZI TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top