• HABARI MPYA

    Monday, April 08, 2019

    SIMBA SC YAILALAMIKIA CAF KUBADILI MAREFA WA MECHI YAO YA MARUDIANO NA MAZEMBE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba SC imelalamikia uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubadili marefa wa mchezo wa marudiano Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyehi, TP Mazembe Jumamosi wiki hii nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Crescentius John Magori ameiandikia barua CAF kulalamikia juu ya uamuzi huo wa ghafla kwa sababu zisizo na mashiko, wakiteuliwa marefa wa nchi jirani na DRC kuchezesha mechi hiyo. 
    Marefa wapya walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo ni mpuliza filimbi Janny Sikazwe, mshika kibendera wa pili, Romeo Kasengele refa wa mezani, Audrick Nkole wote wa Zambia pamoja na mshika kibendera wa kwanza Berhe Tesfagiorgis O'michael wa Eritrea.

    Marefa wa awali ni Bamlak Tessema Weyesa aliyepangwa kupuliza kipyenga, mshika kibendera wa kwanza Temesgin Samuel Atango wote wa Ethiopia, Gilbert Cheruiyot mshika kibendera wa pili na refa wa zamani Peter Waweru wote wa Kenya.
    Simba SC watakuwa wageni wa TP Mazembe Jumamosi Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi wakihitaji ushindi au sare ya mabao kwenda Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kulazimishwa sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza juzi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Simba SC ilicheza vizuri mno Jumamosi na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kukaribia kabisa kuibuka na ushindi Uwanja wa Taifa.    
    Dakika ya 31 mshambuliaji Mnyarwanda wa Simba SC, Meddie Kagere alipiga tik-tak nzuri kuunganisha krosi ya beki wa kulia, Zana Coulibally kutoka Burkina Faso, lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondoshwa kwenye eneo la hatari.
    Nahodha, Bocco akaikosesha timu yake bao la wazi dakika ya 48 baada ya kupiga nje akiwa anatazamana na kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Bocco tena dakika ya 53 akapiga mpira ukambabatiza kipa na kutoka nje baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Bocco akakamilisha siku yake mbaya kwa kukosa penalti dakika ya 59 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere akiwa nje kidogo ya boksi kulia.
    Kwa Mazembe, wao walitengeneza nafasi mbili tu za kusema walikaribia kupata bao, zaidi ya hapo waliutawala tu mchezo.
    Kwanza dakika ya nne mshambuliaji wake, Mkongo Jackson Muleka alipoangushwa na kwenye eneo la hatari la Simba SC, lakini refa Mustapha Ghorbal kutoka Algeria akamuonyesha kadi ya njano akidhani alijiangusha – pale asingeanguka kama angepiga ingekuwa habari nyingine.
    Nafasi nyingine nzuri mno Mazembe walipata dakika ya 89, baada ya mtokea benchi Glody Likonza kupiga shuti lililogonga mwamba wa kulia na kutoka nje akiwa amebaki yeye na kipa, Aishi Salum Manula.
    Zaidi ya hapo refa Mustapha Ghorbal alimaliza mpira wakati Mazembe wanajiandaa kupiga kona kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAILALAMIKIA CAF KUBADILI MAREFA WA MECHI YAO YA MARUDIANO NA MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top