• HABARI MPYA

    Sunday, April 07, 2019

    MILANGO YA NUSU FAINALI LIGI YA MABINGWA IPO WAZI KWA SIMBA

    TIMU ya SIMBA SC jana imelazimishwa sare ya 0-0 na Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC watalazimika kwenda kushinda ugenini kwenye mchezo wa marudiano Aprili 13 Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, au kutoa sare ya mabao ili wafuzu kwa mabao ya ugenini.
    Simba SC ilicheza vizuri mno na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kukaribia kabisa kuibuka na ushindi Uwanja wa Taifa – lakini haikuwa bahati yao, ndivyo unavyoweza kusema.
        
    Dakika ya 31 mshambuliaji Mnyarwanda wa Simba SC, Meddie Kagere alipiga tik-tak nzuri kuunganisha krosi ya beki wa kulia, Zana Coulibally kutoka Burkina Faso, lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondoshwa kwenye eneo la hatari.
    Nahodha, Bocco akaikosesha timu yake bao la wazi dakika ya 48 baada ya kupiga nje akiwa anatazamana na kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Bocco tena dakika ya 53 akapiga mpira ukambabatiza kipa na kutoka nje baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Bocco akakamilisha siku yake mbaya kwa kukosa penalti dakika ya 59 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere akiwa nje kidogo ya boksi kulia.
    Kwa Mazembe, wao walitengeneza nafasi mbili tu za kusema walikaribia kupata bao, zaidi ya hapo waliutawala tu mchezo.
    Kwanza dakika ya nne mshambuliaji wake, Mkongo Jackson Muleka alipoangushwa na kipa Aishi Manula kwenye eneo la hatari la Simba SC, lakini refa Mustapha Ghorbal kutoka Algeria akamuonyesha kadi ya njano akidhani alijiangusha – pale asingeanguka kama angepiga ingekuwa habari nyingine.
    Nafasi nyingine nzuri mno Mazembe walipata dakika ya 89, baada ya mtokea benchi Glody Likonza kupiga shuti lililogonga mwamba wa kulia na kutoka nje akiwa amebaki yeye na kipa, Aishi Salum Manula.
    Zaidi ya hapo refa Mustapha Ghorbal alimaliza mpira wakati Mazembe wanajiandaa kupiga kona kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
    Mchezo ulikuwa mzuri sana kwa Simba SC jana, walichokosa ni bahati tu, kwani walitengeneza nafasi zisizopungua tatu nzuri wakashindwa kufunga. Unasemaje kuhusu ile tiktak ya Kagere, kwa nini iligonga nguzo badala ya kuingia ndani. Na ile penalti kwa nini ilipaa? Hiyo ndiyo soka.
    Kinachotakiwa kwa Simba SC sasa ni kujipanga kwa mchezo wa marudiano ambao utaamua timu ya kwenda Nusu Fanali, kwani bado milango ipo wazi kwao.
    Simba imekwishawahi kufanya maajabu ya kihistoria katika mashindano haya kama kutoka kufungwa 4-0 na Mufurilla Wanderers Dar es Salaam na kwenda kushinda 5-0 Lusaka inaweza kabisa kwenda kushinda Lubumbashi.
    Na ambacho watu wanapaswa kufahamu ni kwamba, kuelekea mchezo wa marudiano, presha ipo zaidi kwa TP Mazembe kuliko Simba SC kwa sababu wanatakiwa kushinda lazima.
    Kwa wanaokumbuka mwaka jana TP Mazembe ilitolewa katika hatua kama hii na C.D. Primeiro de Agosto ya Angola kwa mabao ya ugenini, baada ya kuanza na sare ya 0-0 Luanda na kwenda kutoa sare ya 1-1 Lubumbashi.
    Unaweza kuona ambavyo nafasi ya Simba SC kwenda kuweka rekodi nyingine ya kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kuvitoa vigogo wa Afrika, TP Mazembe ipo wazi. Ni suala la maandalizi na kujipanga tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MILANGO YA NUSU FAINALI LIGI YA MABINGWA IPO WAZI KWA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top