• HABARI MPYA

    Friday, May 19, 2017

    MSUVA: NAKWENDA MWANZA KUONGEZA MABAO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    WINGA wa Yanga, Simon Happygod Msuva amesema anakwenda Mwanza kuongeza mabao ili atimize malengo yake ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu.
    Yanga wanatarajiwa kuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kesho katika mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Dar es Salaam, Msuva alisema kwamba baada ya kuukosa mchezo uliopita kutokana na kuwa majeruhi anataka kumaliza msimu vizuri.
    “Ni mchezo ambao tunakwenda kumalizia msimu, mchezo ambao tunatakiwa kuutumia kuwaaga vizuri mashabiki wetu, lakini pia kwa mtu kama mimi kuutumia pia kuongeza mabao ili nifanikishe azma yangu ya kuwa mfungaji bora,”alisema. 
    Msuva anaongoza kwa mabao yake 14 Ligi Kuu, akifuatiwa na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting mwenye mabao 13 na Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar mabao 12.
    Na akifanikiwa kuchukua tena na msimu huu, Msuva ataweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu mara mbili, baada ya awali kubeba tuzo hiyo msimu wa 2014 – 2015.
    Na atakuwa mchezaji wa pili tu kuchukua tuzo hiyo mara mbili tangu mfumo mpya wa Ligi Kuu kuchezwa ndani ya miaka miwili kuanzia msimu wa 2007 – 2008, mwingine akiwa ni Mrundi, Amissi Tambwe.
    Tambwe ambaye anashikilia tuzo hiyo kwa sasa baada ya kuitwaa msimu uliopita akiwa Yanga, ndiye mfungaji bora pia wa msimu wa 2013 – 2014 akiwa Simba.  
    Simon Msuva (kulia) akipewa maelekezo na kocha wake, George Lwandamina jana azoezini Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 
    WAFUNGAJI BORA LIGI KUU TANGU 2007- 2008
    Msimu           Mchezaji                  Timu             Mabao
    2015 – 2016: Amissi Tambwe Yanga SC 21
    2014 – 2015: Simon Msuva Yanga SC 17
    2013 – 2014: Amissi Tambwe Simba SC 19
    2012 – 2013: Kipre Tchetche Azam FC 17
    2011 – 2012: John Bocco Azam FC 19
    2010 – 2011: Mrisho Ngassa Azam FC 18
    2009 – 2010:  Mussa Mgosi Simba SC 18
    2008 – 2009:  Boniphace Ambani Yanga SC 18
    2007 – 2008:  Michael Katende Kagera Sugar 11
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA: NAKWENDA MWANZA KUONGEZA MABAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top