• HABARI MPYA

  Friday, May 12, 2017

  LUIZIO AIREJESHA SIMBA KILELENI LIGI KUU, APIGA ZOTE MBILI STAND WAFA 2-1 TAIFA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KAMA ilivyotarajiwa, Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United ya Shinyanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 65 baada ya ushindi wa leo wakiwa wamecheza mechi 29, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 62, ambao wanaweza kurudi kileleni kwa mabao zaidi, wakiifunga Mbeya City kesho Uwanja wa Taifa.
  Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Stand United ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa nyota wake, Suleiman Kassim ‘Selembe’ aliyefunga sekunde ya 58 dakika ya kwanza.
  Wachezaji wa Simba (kulia) wakimpongeza Juma Luizio baada ya kufunga, huku wachezaji wa Stand United (kushoto) wakilaumiana 

  Juma Luizio (kushoto) akimpira beki wa Stand United, Ibrahim Job (katikati) leo Uwanja wa Taifa
  Mshambuliaji wa Simba, Laudit Mavugo akipambana na beki wa Stand United, Job Ibrahim
  Winga wa Simba, Shiza Kichuya akimtoka beki wa Stand United leo Uwanja wa Taifa

  Mchezaji huyo wa zamani wa Azam FC ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga, alifunga bao hilo akitumia makosa ya kiungo anayechezeshwa beki ya kati kwa sasa kutokana na uhaba wa nafasi hizo, Mghana James Kotei.
  Na ikawa rahidi kwa kiungo huyo, Selembe kufunga baada ya kipa Mghana, Daniel Agyei naye kuvutika kutoka langoni, hivyo Mzanzibari huyo akanyunyiza mpira nyavuni kiulaini.
  Simba walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa mshambuliaji wake, Juma Luizio anayecheza kwa mkopo kutoka Zesco United ya Zambia, aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya winga Shiza Kichuya.
  Juma Luizio tena akawainua vitini mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la pili na la ushindi dakika ya 35, kwa mara nyingine akimalizia kazi nzuri ya Kichuya.
  Kipindi cha pili milango ilikuwa migumu kwa pande zote mbili na Simba ikafanikiwa kuvuna pointi tatu kwa ushindi wa 2-1 na kurejea kileleni.
  Kikosi cha Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, James Kotei, Shiza Kichuya/Abdi Banda dk78, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Juma Luizio/Pastory Athanas dk61, Jonas Mkude na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Mwinyi Kazimoto dk51.
  Stand United; Frank Muwonge, Aaron Lulambo/Rajab Rashid dk81, Jacob Massawe, Miraj Maka, Revocatus Richard, Erick Mulilo, Adam Salamba, Kheri Khalifa/Sixtus Sabilo dk70, Frank Khamis, Ibrahim Job na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LUIZIO AIREJESHA SIMBA KILELENI LIGI KUU, APIGA ZOTE MBILI STAND WAFA 2-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top