• HABARI MPYA

    Saturday, February 18, 2017

    MSUVA AMUAHIDI ZAWADI MANJI LEO, NI ‘KUISHINDILIA MIBAO’ NGAYA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    WINGA wa Yanga, Simon Msuva amesema leo watampa zawadi Mwenyekiti wao, Yussuf Manji baada ya misukosuko aliyoipata kwa wiki nzima.
    Yanga leo inamenyana na Ngaya de Mde katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Msuva amesema wataipa kipigo kitakatifu timu hiyo kumfariji Manji. 
    “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, hadi hapa tulipo tupo vizuri na tunafurahi zaidi Mwenyekiti wetu (Manji) ametoka kwa dhamana kwa hiyo tutampa zawadi nzuri kwa kuwafunga Ngaya,”alisema Msuva.
    Simon Msuva amemuahidi zawadi nzuri Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji leo


    Kuifunga mabao mengi Ngaya leo, itakuwa ‘ulafi’ tu kwa Yanga, kwani tayari ina hazina ua ushindi wa mabao 5-1 ugenini katika mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita.
    Na Manji aliachiwa kwa dhamana juzi mchana baada ya kusomewa shitaka la tuhuma za kutumia dawa za kulevya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
    Baada ya kusoma shitaka hilo, Hakimu Cyprian Mseha alimtaka mtuhumiwa huyo kufika mahakamani hapo Machi 16 kwa mwendelezo wa kesi hiyo.
    Manji aliwasili mahakamani chini ya ulinzi wa Polisi, akitokea kituo kikuu cha Polisi, Dar es Salaam alikuwa amewekwa rumande tangu Alhamisi.
    Hata hivyo, Jumamosi mchana Manji alipelekwa hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam baada ya hali yake kubadilika na kuwa mbaya ikiwelezwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo.
    Taarifa zilisema Manji alifanyiwa upasuaji mdogo na kurejeshwa Polisi jana, kabla ya jana kupandishwa kizimbani. 
    Manji aliwekwa rumande baada ya kujisalimisha mwenyewe kituo kikuu cha Polisi Alhamisi iliyopita, baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu 65 wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
    Japokuwa Manji na wengine wote 64 waliotajwa walitakiwa kuripoti Polisi Ijumaa, lakini yeye alijipeleka mwenyewe Alhamisi pamoja na Askofu Gwajima, ambaye aliachiwa baada ya siku mbili.
    Na wakati tuhuma zake zikibadilika kutoka kwenye kushukiwa kuuza hadi kudaiwa anatumia dawa za kulevya, Manji pia anakabiliwa na shitaka lingine kupitia kampuni yake ya Quality Group Limited, kuajiri wageni bila vibali vya kufanya kazi nchini.
    Ofisa wa Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule, alisema Jumanne wiki hii kwamba Manji anatakiwa kufika ofisini hapo kujibu mashitaka ya kuajiri watu 25, ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini. 
    Msumule alisema ilikuwa wamkamate Manji Jumatatu wiki hii, lakini wakaambiwa amelazwa hospitali, hivyo wameacha maagizo akitoka hospitalini aripoti mwenyewe Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Dar es Salaam.
    Msumule alisema kwamba walifanikiwa kukamata pasipoti 126 zenye makosa Jumamosi na kati ya hizo, 25 zilikuwa za waajiriwa ambao hawana vibali.
    Kiingilio cha chini katika mchezo wa leo ni Sh. 3,000, VIP A Sh 20,000, VIP B Sh 10,000 na VIP C Sh 10,000 na mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka Uganda ambao ni Alex Muhabi Nsulumbi atayekapuliza filimbi uwanjani, akisaidiwa na washika vibendera Ronald Kakenya na Lee Okello.
    Refa wa Akiba atakuwa Brian Nsubuga Miro huku Kamishna akitokea Afrika Kusini ambaye ni Monnyenyone Lucas Nhlapo na mshindi atakutana na mshindi kati ya Zanaco ya Zambia na APR ya Rwanda katika Raundi ya Kwanza. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AMUAHIDI ZAWADI MANJI LEO, NI ‘KUISHINDILIA MIBAO’ NGAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top