• HABARI MPYA

  Tuesday, February 14, 2017

  MANJI APEWA KESI NYINGINE, UHAMIAJI WANAMSUBIRI WAMUWEKE LUPANGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Manji ambaye kwa sasa amelazwa hospitali ya Muhimbili ametakiwa kuripoti Ofisi ya Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam mara atakapotoka hospitalini hapo.
  John Msumule, Ofisa Uhamiaji Dar es Salaam amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba Manji anatakiwa kufika ofisini hapo kujibu mashitaka ya kuajiri watu 25, ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini. 
  Msumule amesema ilikuwa wamkamate Manji jana, lakini wakaambiwa amelazwa hospitali, hivyo wameacha maagizo akitoka hospitalini aripoti mwenyewe Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Dar es Salaam.
  Yussuf Manji ametakiwa kuripoti Ofisi ya Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam mara atakapotoka hospitalini alikolazwa

  Msumule alisema kwamba walifanikiwa kukamata pasipoti 126 zenye makosa Jumamosi na kati ya hizo, 25 zilikuwa za waajiriwa ambao hawana vibali.
  “Wote hawa hatua zitachukuliwa na watapelekwa mahakamani, lakini lazima niseme ukweli, hawa hawatapelekwa peke yao Mahakamani, lazima Yussuf Manji, ambaye ndiye mwajiri wa watu hawa, ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hii, lazima afikishwe mahakamani kujibu shitaka la kuajiri watu wageni wasio na vibali,”. 
  “Jana ilikuwa tumkamate alale mahabusu na leo tumempeleke mahakamani, bahati mbaya wakati tunafanya zoezi la kwenda kumkamata, tukapewa taarifa kwamba amelazwa hospitalini hadi sasa, mara tu atokapo, aripoti haraka ofisi hii ili tumuunganishe kwenye kesi hii ya kuwaajiri watu wasio na vibali,”. 
  “Hatutajali ukubwa wa hela yako, hatutajali cheo chako cha mahali popote pale, hatutajali kwa njia yoyote ile, una mamlaka gani katika nchi ya Tanzania, utakamatwa, utawekwa ndani, utajibu mashitaka,”alisema.
  Manji alimbizwa hospitali juzi kutoka kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam alipokuwa anashikiliwa kwa mahojiano ya tuhuma za kujihusisha na biashara za dawa za kulevya. Na hiyo ilifuatia kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu 65 wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo Jumatano iliyopita.
  Japokuwa Manji na wengine wote 64 waliotajwa walitakiwa kuripoti Polisi Ijumaa, lakini yeye alijipeleka Alhamisi na akawekwa ndani ambako alilala hadi Jumamosi alipokimbizwa hospitali mchana.
  Na wakati tuhuma zake za kujihusisha na biashara za dawa za kulevya zikiwa hazijapatiwa ufumbuzi, Manji anaingia hatiani kwa kuajiri wageni wasio na vibali.
  Wazi hilo ni pigo kwa klabu ya Yanga ambayo kwa sasa inamtegemea kwa kila kitu Manji, kwani mbali na kuwa Mwenyekiti wa klabu, pia ndiye mfadhili na mdhamini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANJI APEWA KESI NYINGINE, UHAMIAJI WANAMSUBIRI WAMUWEKE LUPANGO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top