• HABARI MPYA

    Wednesday, February 01, 2017

    KIUNGO FUNDI ALIYEWIKA YANGA GEOFFREY BONNY YU MAHUTUTI KWAO IRINGA, ANAHITAJI MSAADA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Geoffrey Bonny Namwandu (37) yu mahututi nyumbani kwao Iringa akisumbuliwa na maradhi ya homa ya matumbo na Malaria.
    Dada wa mchezaji huyo wa zamani wa Prisons ya Mbeya na Yanga SC ya Dar es Salaam, Neema ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba hali ya kaka yake ni mbaya na anahitaji msaada ili apelekwe hospitali kubwa akapatiwe tiba ya kuokoa maisha yake.
    Neema amesema kwamba Bonny alifanyiwa vipimo katika hospitali ya Makandana ya wilaya ya Rungwe na wamesema ni Malaria na homa ya matumbo vinamsumbua.
    Geoffrey Bonny hali yake ni mbaya nyumbani kwao Iringa na anahitaji msaada

    Neema amesema Bonny anapatiwa matibabu nyumbani kwa sababu hawana uwezo wa kifedha wa kumpeleka hospitali.
    Na akaomba walio tayari kumsaidia wawasiliane naye kwa namba za simu + 255 765 359 290 ili kuokoa maisha ya shujaa huyo wa zamani wa taifa.
    Bonny alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars enzi za kocha Mbrazil, Marcio Maximo na wengi wanamkumbuka kwa soka yake maridadi katika sehemu ya kiungo, licha ya kwamba aliibuliwa wakati umri wake umekwishaenda.
    Alicheza Yanga chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic na akaendelea hata alipoondolewa mwalimu huyo na kuletwa Mseribia mwingine, Kostadin Papic.
    Timu ya mwisho ya Geoffrey Bonny kuchezea, Simrik SYC ya Nepal      
    Geoffrey Bonny (wa pili kulia waliosimama)  akiwa kwenye kikosi cha Simrik SYC ya Nepal. Wa pili kushoto waliosimama ni mchezaji mwingine wa Tanzania, Pius Kisambale  
    Geoffrey Bonny akiichezea Taifa Stars kwenye michuano ya CHAN mwaka 2009

    Ni kati ya wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kukata tiketi ya kucheza fainali pekee za michauno ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.  
    Hata hivyo, Maximo akamtema katika kikosi cha Stars baada ya fainali za CHAN nchini Ivory Coast mwaka 2009 kutokana na kuwa majeruhi.
    Maumivu hayo yalimfanya aachwe na Yanga mwaka 2011 akaenda kumalizia soka yake Simrik SYC ya Nepal.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIUNGO FUNDI ALIYEWIKA YANGA GEOFFREY BONNY YU MAHUTUTI KWAO IRINGA, ANAHITAJI MSAADA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top