• HABARI MPYA

    Friday, August 19, 2016

    KESSY ATAKIWA KUILIPA SIMBA MILIONI 120 AANZE KUCHEZEA YANGA WAKATI WOWOTE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Yanga, Hassan Ramadhani Kessy ametakiwa kuilipa klabu yake ya zamani, Simba SC Sh. Milioni 120 ili aanze kuichezea timu yake mpya katika mashindano kuanzia sasa.
    Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyoketi jana chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Richard Sinamtwa imemtaka beki huyo kuilipa klabu ya zamani, Simba SC kwa kuvunja Mkataba.
    Habari za ndani kutoka TFF zimesema kwamba Kamati imejiridhisha kwamba Kessy alivunja Mkataba na Simba kinyume cha utaratibu hivyo anapaswa kuilipa Simba.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro akiwatambulisha Hassan Kessy na Juma Mahadhi (kulia) Mei 25 mwaka huu kabla ya fainali ya Kombe la TFF baina ya timu yake na Azam FC
    Na habari zaidi zinasema kwamba, katika Mkataba wake na Smba, wote klabu na mchezaji walikubaliana atakayeuvunja atalipa dola za Kimarekani 60,000 zaidi ya Sh. Milioni 120,000 za Tanzania.
    Kessy alisajiliwa na Simba SC misimu miwili iliyopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa Mkataba wa miaka miwili akilipwa Sh. Milioni 20. 
    Na akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Meneja wa Kessy, Athumani Tippo amesema anashangazwa na uamuzi wa Kamati kumtaka Kessy ailipe Simba.
    Tippo alisema Mkataba wa Kessy na Simba uliisha Juni 17 na beki huyo wa kulia akasaini Yanga SC Juni 21, baada ya kuzungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei.   
    “Kilichotokea baada ya habari za Kessy kutaka kuhamia Yanga kuvuja, Mei 25 mwaka huu alipokwenda kwenye mechi ya fainali ya Kombe la TFF dhidi ya Azam mashabiki wakamvisha jezi ya Yanga,”.
    “Hakuvishwa na klabu ya Yanga, ni mashabiki. Sasa huwezi kusema Kessy alivunka Mkataba na Yanga kinyume cha utaratibu,”alisema Tippo.
    Pamoja na hayo, Tippo alisema kwamba amepeleka malalamiko Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA) ili waweze kumsaidia mchezaji huyo katika sakata hilo.
    Na Yanga tayari wameweka msimamo wa kutokuwa tayari kulipa Sh. Milioni 120 ambazo Simba wanataka ili Kessy acheze – maana yake beki huyo mwenye mwili mdogo ataendelea kukaa jukwaani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KESSY ATAKIWA KUILIPA SIMBA MILIONI 120 AANZE KUCHEZEA YANGA WAKATI WOWOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top