• HABARI MPYA

    Saturday, April 08, 2017

    YANGA KUMKOSA TAMBWE MECHI NA MC ALGER LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC itaendelea kumkosa mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe katika mchezo wa leo dhidi ya Mouloudia Club Alger ya Algeria.
    Mabingwa hao wa Tanzania, wanateremka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na timu kutoka Algeria katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 
    Tambwe aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya goti tangu Januari, amepona na ameshiriki mazoezi na wenzake kwa wiki yote hii, lakini ameomba wiki moja zaidi ili awe fiti kikamilifu kabla ya kurejea kuipigania timu yake kwenye vita ya mataji.
    Amissi Tambwe (kushoto) amefanya mazoezi wiki yote hii, lakini hayuko tayari kwa mchezo wa leo
    MC Alger wamefanya mazoezi Uwanja wa Taifa jana baada ya kuwasili Alhamisi

    Pamoja na Tambwe, Yanga itaendelea kumkosa kiungo Mzambia, Justin Zulu aliyeumia ugoko baada ya kugongwa na Himid Mao wa Azam Aprili 1, ambaye anatarajiwa kufunguliwa nyuzi kesho kabla ya kuanza mazoezi Jumatatu, maana yake anaweza kuwa fiti kwa mchezo wa marudiano Aprili 15 mjini Algiers.
    Lakini habari njema ni kwamba Wazimbabwe wawili waliokuwa majeruhi, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma wamepona na leo wanaweza kucheza. 
    Mchezo huo unaotarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni, utachezeshwa na marefa kutoka Rwanda, Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka, wakati refa wa akiba atakuwa Ruzindana Nsoro na Kamisaa ni Ata Elmanan Hassan Osama kutoka Sudan. 
    Yanga wamekuwa katika maandalizi ya mchezo huu kwa wiki nzima tangu waifunge Azam 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi iliyopita, bao pekee la Mzambia, Obreu Chirwa Uwanja wa Taifa.
    Wakati Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Tiffany makutano ya barabara ya Morogoro na Mtaa wa Indira Gandhi, wapinzani wao MC Alger waliwasili juzi Saa 3.30 usiku kwa ndege maalumu ya kukodi na kufikia Hoteli ya Holiday Inn, katikati ya Jiji.
    Jana jioni Waarabu hao walifanya mazoezi Uwanja wa Taifa na wachezaji wake walionekana wachangamfu pamoja na hali ya baridi na mvua za rasha rasha.  
    Viingilio katika mchezo huo ni Sh 30,000 kwa VIP ‘A’; Sh 20,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ wakati mzungunguko itakuwa ni Sh 3,000.
    Wakati Yanga SC, imeangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia katika Ligi ya Mabingwa, MC Alger imefika hatua hii kwa kuitoa Renaissance ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Hatua hii hukutanisha timu zinazotolewa Ligi ya Mabingwa dhidi ya zinazofuzu hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho na Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 0-0 Lusaka, hivyo kutolewa kwa mabao ya ugenini, wakati MC Alger ilishinda 2-0 nyumbani na kwenda kufungwa 2-1 Kinshasa, hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-2.
    Mwaka jana pia Yanga ilitolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa na kuangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ambako iliitoa Sagrada Esperanca ya Angola.  
    Kila la heri wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya Afrika. Mungu ibariki Yanga. Mungu ibariki Tanzania. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KUMKOSA TAMBWE MECHI NA MC ALGER LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top