• HABARI MPYA

    Wednesday, May 13, 2015

    ULIMWENGU AMWAMBIA NGASSA; “KAZA MWANANGU UTOKE, NDIYO CHANELI ZENYEWE HIZO”

    Na Mahmoud Zubeiry, BETHLEHEM
    MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Thomas Emmanuel Ulimwengu (pichani kushoto) amemuambia mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ajibidiishe baada ya kusajiliwa Free State Stars ya Afrika Kusini ili kusaka mafanikio zaidi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu leo kutoka Lubumbashi, DRC, Ulimwengu amesema kwamba amefurahishwa mno na Ngassa kupata timu Afrika Kusini.
    “Kwa kweli nimefurahi sana, Ngassa ni mchezaji mzuri sana ambaye siku zote nilikuwa najiuliza kwa nini anapoteza muda wake Tanzania. Nampongeza kwa mafanikio haya na ninamtakia kila la heri,”amesema.
    Ulimwengu amemuambia Ngassa anapaswa kuongeza bidii ili kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwa ajili ya kusaka mafanikio zaidi.
    “Yaani asione kama pale ndiyo amefika. Afanye bidii kwanza awe nyota na tegemeo la timu na baada ya hapo timu nyingine zenye kutoa maslahi bora zaidi zimfuate, hapo atakuwa amekuza soko lake,”amesema Ulimwengu.
    Baada ya kusaini Mkataba wa miaka minne na Free State jana, Ngassa ataondoka mjini Bethlehem kesho mapema asubuhi kwenda Rusenburg, kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mashindano ya Kombe la COSAFA yanayoanza Jumapili mjini humo.   
    Taifa Stars imepangwa pamoja na Namibia, Lesotho na Zimbabwe katika Kundi A, wakati Kundi B lina timu za Shelisheli, Madagascar, Mauritius na Swaziland.
    Kila timu itakayoongoza kundi, itaungana na wenyeji Afrika Kusini, Botswana, Ghana na Malawi, Msumbuji na Zambia kwa ajili ya hatua ya Robo Fainali.
    Ngassa kulia akiwa na Meneja wa Free State Stars, Mutouba Mokoena kushoto

    Mpinzani wa Tanzania katika hilo, anatarajiwa kuwa Zimbabwe, ambaye hata hivyo alitolewa na Taifa Stars katika mechi za kufuzu AFCON mwaka jana.
    Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi, Msumbuji na Zambia zimeingia moja kwa moja katika Robo Fainali kwa sababu zipo juu viwango vya ubora wa soka vya FIFA.
    Kombe la COSAFA lilianza mwaka 1997 linajumuishaa nchi 16 wanchama kutoka Kusini mwa Bara la Afrika, limekua likifanyika kwa kushirikisha nchi wanachama waliopo Kusini mwa bara la Afrika.
    Nchi wanachama wa COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoro, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mayotte, Msumbuji, Namibia, Reunion, Shelisheli, Swaziland, Zambia na Zimbabwe, lakini katika kuiongezea ladha ya ushindani, sasa hivi zinaalikwa na timu kutoka nje ya ukanda huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU AMWAMBIA NGASSA; “KAZA MWANANGU UTOKE, NDIYO CHANELI ZENYEWE HIZO” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top