• HABARI MPYA

    Friday, May 31, 2013

    USAJILI SIMBA SC SWAAAFI....OLOYA KWA ASILIMIA 80 ANATUA MSIMBAZI

    Anakuja; Moses Oloya kwa asilimia 80 safi kuja Msimbazi
    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 31, 2013 SAA 4:40 ASUBUHI
    SIMBA SC imekamilisha usajili wa kikosi cha msimu ujao kwa asilimia 80 na ndani yake itakuwa na wachezaji wanne wa kigeni, akiwemo mshambuliaji Moses Oloya kutoka Uganda.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wamekamilisha mazungumzo na kufikia makubaliano na Oloya, na sasa kuna kitu kimoja wanasubiri kabla ya kusaini naye mkataba.
    “Timu ya taifa ya Uganda itacheza na Liberia mechi za kufuzu za Kombe la Dunia. Akimaliza anakwenda kwenye klabu yake kuchukua barua ya kututhibitishia hana mkataba, ndipo tutampa chake naye asaini,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).    
    Kiungo huyo mshambuliaji wa The Cranes, yaani ndege aina ya Korongo aliyezaliwa miaka 20 iliyopita anamaliza mkataba wake na Saigon Xuan Thanh ya Vietnam Agosti mwaka huu, lakini ameamua kuuvunja kutokana na klabu hiyo kukiuka mambo ya msingi katika mkataba huo.
    Mkoba; Ssenkoom ametua Simba SC

    Anadai klabu hiyo haijamlipa mshahara kwa zaidi ya miezi mitatu, hivyo pekee hiyo inahalalisha uvunjwaji wa mkataba baina yao naye kutua Msimbazi kama mchezaji huru.
    Simba ikimpata mchezaji huyo aliyekwenda Vietnam akitokea KCC ya kwao, aliyoichezea tangu 2009 hadi 2010, itakuwa imelamba dume.
    Oloya ni mchezaji mzuri kuliko Emmanuel Okwi ambaye Simba SC imemuuza Etoile du Sahel ya Tunisia na Desemba mwaka jana, Yanga SC na Azam zote zilijaribu kutaka kumsajili bila mafanikio.
    Mwishowe Azam ikaona bora kumsajili Brian Umony, wakati Yanga ilibanwa na nafasi ya idadi ya wachezaji wa kigeni, lakini ikamuweka kwenye orodha ya wachezaji inayoweza kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.
    Mbali na Oyola, wachezaji wengine wa kigeni wa ndani ya Simba watakuwa Waganda watupu, kipa Abbel Dhaira, beki Samuel Ssenkoom na kiungo Mussa Mudde, maana yake klabu hiyo ina nafasi moja ya mchezaji wa kigeni kwa mujibu wa kanuni.
    Katika mazoezi ya Simba yanayoendelea kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam, chini ya kocha mpya Abdallah Athuman Seif ‘King Kibaden’ wamejitokeza wachezaji zaidi ya 20 kufanya majaribio, wakiwemo kutoka Nigeria, DRC, Senegal, Ivory Coast na Msumbiji mbali ya wazawa.
    Adeyoum Saleh Ahmed, beki wa kushoto timu ya taifa ya Zanzibar na klabu ya Miembeni ya Zanzibar ni kati ya wachezaji ambao wamekuwa kivutio katika mazoezi hayo.
    Tayari Simba SC imewasajili moja kwa moja wachezaji wanne wazawa, kipa Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar, kiungo Twaha Shekuwe ‘Messi’ kutoka Coastal Union na mshambuliaji Zahor Pazi kutoka Azam FC, aliyekuwa anacheza kwa mkopo JKT Ruvu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: USAJILI SIMBA SC SWAAAFI....OLOYA KWA ASILIMIA 80 ANATUA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top