• HABARI MPYA

  Ijumaa, Mei 31, 2013

  KUELEKEA TUZO ZA KILI 2013 KIKWETUKWETU; UPI WIMBO BORA WA HIP HOP?

  Na Princess Asia, IMEWEKWA MEI 31, 2013 SAA 4:30 ASUBUHI
  ZOEZI la upigaji wa kura za tuzo za wanamuziki bora Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Award lililoanza Mei 2, mwaka huu linazidi kupamba moto kwa wapenzi wa muziki kuwapigia kura wasanii wawapendao.
  Jana kwa muhtasari tulielezea ushindani uliopo katika kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana ambako Chuki Bure, Mapito, Me n U, Sihitaji Marafiki na Single Boy zinashindanishwa. 
  Leo tunahamia kwenye Wimbo Bora wa Hip hop ambako Alisema wa Stamina na Jux, Bum Kubam wa Nikki wa Pili na G Nako, Dear God wa Kalla Jeremiah, Nasema Nao wa Nay wa Mitego na Sihitaji Marafiki wa Fid Q zinashindanishwa. 
  Kwa ujumla nyimbo zote zilizoingia fainali ni ambazo mwaka jana zilifanya vizuri katika medani ya muziki nchini kiasi cha kujipatia umaarufu mkubwa. 
  Hakika kuna ushindani mkubwa katika vipengele hivi na zaidi wimbo utabebwa na idadi ya kura utakazopigiwa na mashabiki wake ili kushinda tuzo hiyo. 
  Wapiga kura wanatakiwa kuandika namba ya msanii, wimbo, kikundi au bendi anayotaka ishinde na kisha kutuma kwenda namba 15346, wakati njia nyingine zaidi ya ujumbe mfupi (SMS) ni pamoja na Email, kwenda ktma@innovex.co.tz au kutembelea tovuti ya www.kilitimetz.com na kupiga kura moja kwa moja.
  Meneja wa Bia Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, wamejiandaa vizuri mwaka huu kuhakikisha zoezi linafana.
  Kilele cha sherehe za utoaji tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards zilizobeba kaulimbiu ya Kikwetu kwetu ni Juni 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, ambako pamoja na wasanii mbalimbali kupokea tuzo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pia. 
  Je, katika kipengele vya Wimbo Bora wa Hip hop, utatoa wapi kura yako?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KUELEKEA TUZO ZA KILI 2013 KIKWETUKWETU; UPI WIMBO BORA WA HIP HOP? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top