• HABARI MPYA

  Jumatatu, Mei 27, 2013

  RASMI 'KING KIBADEN' KOCHA MPYA SIMBA SC, AANZA KAZI KESHO KINESI

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 27, 2013 SAA 9:35 ALASIRI
  ANGALAU sasa unaweza kumhesabu Abdallah Athumani Seif maarufu kama King Kibadeni ni kocha mpya wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam baada ya kufikia makubaliano katika kikao cha leo mchana na uongozi wa klabu hiyo.
  Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala sasa anaandaa Mkataba kulingana na makubaliano na Kibadeni aliyekuwa kocha wa Kagera Sugar msimu uliopita Bukoba, kisha ataupeleka kwa Kamati ya Utendaji ya klabu ukapitiwe tayari kwa gwiji huyo wa Msimbazi kuusaini Jumatano.
  Amerudi nyumbani; Abdallah Kibadeni
  kocha mpya Simba SC

  Lakini wakati taratibu za Mkataba zikiendelea, Kibadeni au Chifu Mputa ataanza kazi kesho saa 1:00 asubuhi katika Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam.
  Asubuhi ya kesho, Kibadeni atawafanyia usajili wachezaji zaidi ya 40 wakiwemo kutoka nje ya Tanzania ambao wanaomba kusajiliwa na mabingwa hao wa zamani wa Afrika Mashariki na kati na Tanzania Bara.
  Baada ya usaili huo, wachezaji ambao watamvutia mfalme huyo wa mabao wa zamani nchini, wataunganishwa na wachezaji waliosajiliwa Simba SC kwa ajili ya msimu ujao kuanza rasmi maandalizi ya msimu mpya Jumatano, Uwanja wa Kinesi.
  Mazoezi ya Jumatano yatahusisha wachezaji wote, ambao hawapo katika timu zao za taifa, yaani waliokuwepo kwenye kikosi cha msimu uliopita na wapya waliosajiliwa.
  Wachezaji ambao hawatahusika katika programu ya msimu mpya ya Simba SC ni Haruna Moshi ‘Boban’, Amir Maftah, Wilbert Mweta waliomaliza mikataba, Paul Ngalema, Abdallah Juma walioomba kuondoka, Salim Kinje anayetolewa kwa mkopo, Juma Nyosso na Ramadhan Chombo ‘Redondo’, ambao suala lao lipo kwa Kamati ya Utendaji.
  Katika benchi la Ufundi, Kibadeni atakuwa anasaidiwa na walimu wawili, Mganda Moses Basena na mzalendo Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, wakati Meneja atakuwa Nico Njohole na mtunza vifaa atakuwa Ally Cheche.
  Mtihani wa kwanza wa Kibadeni unatarajiwa kuwa nchini Sudan mwishoni mwa mwezi ujao, ambako Simba itacheza Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame pamoja na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
  Simba SC imepangwa Kundi A katika michuano hiyo pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda, wakati Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wamepangwa Kundi C na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na  Vital 'O'  ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda
  Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
  Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, wakati mabingwa watetezi, Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji Juni 20 kwa kumenyana na Express na mechi zote zitachezwa Elfashar.
  Wazee wa 6-0; Kibadeni wa tatu kutoka kushoto akiwa na kikosi kilichofinga Yanga 6-0 1978

  WASIFU WA KING KIBADEN

  1949- Oktoba 11; Alizaliwa Mbagala Kiburugwa Dar es Salaam.
  1959- Alitungwa jina Kibadeni na watoto wenzake kutokana kucheza soka ya nguvu akiwa mdogo na mfupi, ambalo limefunika jina lake halisi la Abdallah Athumani Seif. Mwenyewe anasema Kibadeni maana yake ni kitu cha baadaye. Kwamba kila siku alikuwa akionekana bado kwa umri na umbo wakati anaweza soka.
  1969- Februari 2; Alijiunga na Simba SC ikiitwa Sunderland akitokea Kahe Republic ya Mtaa wa Kongo na Mchikichi, Kariakoo.
  1974- Alifunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Hearts Of Oak ya Ghana nchini Ghana katika Robo Fainali ya Kwanza ya Klabu Bingwa Afrika.
  1974- Aliiongoza Simba kuwa klabu ya kwanza na pekee Tanzania kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika hadi sasa.
  1975- Aliiongoza Simba kuwa klabu ya kwanza kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Dar es Salaam.
  1977- Alifunga mabao matatu peke yake katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Yanga SC.
  1993- Aliiwezesha Simba SC kufika Fainali ya Kombe la CAF akiwa Kocha, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo ikiwa ni miaka 20 baadaye
  1978-Aling’atuka Simba SC na kwenda kuwa kocha mchezaji Majimaji ya Songea.
  2011- Alikwenda Hijja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RASMI 'KING KIBADEN' KOCHA MPYA SIMBA SC, AANZA KAZI KESHO KINESI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top