• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 23, 2013

  HAPA NDIPO SIMBA HUWA WANAJICHUKULIA 'POINTI ZA CHEE' DHIDI YA YANGA SC...

  Mambo ya Simba SC; Ngassa alipotambulishwa Simba alipewa jezi yenye nambana aliyokwenda kuitumia katika timu hiyo. Anyemkabidhi jezi ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange 'Kaburu'

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 23, 2013 SAA 12:30 ASUBUHI
  JUMATATU wiki hii, Yanga SC ilimtambulisha rasmi kiungo wake mshambuliaji, Mrisho Khalfan Ngassa kurejea katika timu hiyo baada ya miaka mitatu tangu mwaka 2010 alipoondoka.
  Ikumbukwe Ngassa aliondoka Yanga mwaka huo akienda Azam FC, alipocheza kwa miaka miwili kabla ya kuhamia Simba SC ambako alicheza karibu mwaka mmoja kabla ya kurejea Yanga SC mapema wiki hii.
  Ilikuwa si hafla, bali mkutano tu na Waandishi wa Habari kumtangaza mchezaji huyo, tena katika ukumbi ambao hauna mvuto wala hadhi ya kuitwa ukumbi wa mikutano, hususan kwa klabu kubwa kama Yanga.
  Jezi aliyopewa Yanga Jumatatu japokuwa ilikuwa ina jina lake, lakini haikuwa na namba. Anayemkabidhi ni Katibu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako

  Sehemu ndogo iliyojibana bana, iliyopambwa kwa viti sawa za vile vya baa za uswahilini, viongozi mamilionea wa Yanga SC kama Seif Ahmed ‘Magari’, Mussa Katabaro, Abdallah Bin Kleb na Francis Kifukwe walimtambulisha Ngassa kwa mbwembwe zote.
  Achana na hiyo, hata Mwenyekiti wao, Alhaj Yussuf Manji hukutana na Waandishi na wanachama na hata Kamati yake ya Utendaji kwenye ‘kaukumbi hako’- kichekesho zaidi ni jezi ambayo alikabidhiwa Ngassa.
  Tazama hii jezi...

  Katika Mkutano huo, Bin Kleb alisema wamekuwa kwenye mazungumzo na Ngassa kwa takriban miezi sita hadi wanafikia makubaliano na akasaini kabla ya kuamua kumtambulisha.
  Ni sawa na hii aliyovaa Kevin Yondan hapa katika mechi dhidi ya Simba SC, ambayo Yanga wamevaa msimu wote huu?  

  Lakini hakukuwa na dalili za kwamba ulikuwa mpango wa muda mrefu, ilikuwa kama watu wamekurupushwa ndani ya muda mfupi waandae utaratibu wa kumtambulisha Ngassa.
  Huo ni ubabaishaji ambao pengine umezoeleka kwa klabu zote, ingawa kwa kweli zinapaswa kubadilika ili kwenda na wakati kwa kuzingatia kufana kwa tukio ndio picha nzuri.
  Ajabu ni jezi ambayo Ngassa alikabidhiwa- haikuwa aina ya jezi ambazo Yanga wanatumia kwa sasa. Ilikuwa sawa kabisa na zile jezi ambazo mashabiki wananunua mtaani na kuvaa kwenye mechi za timu hiyo.
  Ukiitazama hii na hiyo ya chini hapo, Ngassa akiichezea Simba SC dhidi ya Coastal Union huwezi kuona tofauti.   Japokuwa ilikuwa imeandikwa Ngassa- lakini bado haikuwa jezi ya wachezaji wa Yanga ambazo tumeshuhudia msimu wote huu wakivaa, bali ni sawa na jezi za mashabiki.
  Utambulisho wa mchezaji kwa kukabidhiwa jezi baada ya kusajiliwa ni mfumo wa kisasa, lakini ajabu Yanga SC wanachukulia kama jambo la mzaha tu.
  Mchezaji anaposajiliwa, anakabidhiwa jezi halisi ya timu na ambayo ndiyo atakuwa akiitumia pengine kwa muda wote wa kuwapo kwake katika timu akiutumikia mkataba alioingia na klabu. Haikuwa hivyo kwa Ngassa.
  Na hii ni tofauti sana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC. Ukweli, bila kupepesa macho, Simba SC wanajua kufanya mambo kisasa na kwa usahihi.
  Mfano ni wakati wa kumtambulisha kwao huyo huyo Ngassa baada ya kumsajili, Agosti mwaka jana- walimkabidhi jezi ambayo ilikuwa inatumika katika timu hiyo wakati huo na namba 16, ambayo aliivaa msimu mzima, kasoro mechi moja ya mwisho, dhidi ya Yanga alipovaa jezi namba nane. 
  Si katika hilo tu, kwa mambo mengi Simba SC wanaizidi Yanga katika kwenda kisasa. Wana lile tamasha lao la kila mwaka, Simba SC Media Dar, huwa linafana.
  Wanafanya sherehe kuanzia mchana, jioni wanatambulisha wachezaji wao wote waliosajiliwa kwa mbwembwe za kuvutia, akiitwa mmoja kutokea chumba cha kubadilishia nguo kuingia uwanjani tayari kucheza ya kuzindua msimu mpya wa timu.
  Hata mwaka jana lilifana- haswa pale walipomtambulisha Mbuyu Twite kupitia kwenye TV kubwa la Uwanja wa Taifa na kuonyesha jezi yake- ingawa wakati huo mwenyewe alikuwa Rwanda.
  Kwa Mbuyu, Simba SC kupitia Mwenyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage walimsainisha mkataba na kumpa fedha, lakini kabla hajakamilisha mambo yote muhimu, akarejea Dar es Salaam kutoka Kigali kuja kuwatambia watani.
  Yanga SC walipogundua mapungufu yaliyokuwapo, wakatumia mwanya huo kwenda kumbadili mawazo beki huyo akasaini kwao na kurudisha fedha alizopewa na Rage.
  Lakini bado haipotezi ukweli wa Simba SC kujua kufanya mambo yao kisasa. Simba SC wanajua kufanya mambo ya hisani ili kujiweka karibu na jamii, kama vile kutembelea wagongwa, vituo vya watoto yatima na kuwafariji kwa misaada na kadhalika.   
  Ni mambo madogo madogo tu, lakini yana maana kubwa sana. Unakuwa na timu ya wachezaji wazuri wa gharama, lakini hauna hata ukumbi wa maana wa mikutano.
  Simba SC nao japokuwa wanajua kufanya mambo yao kisasa, lakini wamefeli katika suala la ukumbi wa mikutano.
  Yanga wana ofisi nzuri kidogo zilizo katika mpangilio mzuri, kuanzia ya Katibu, Mhasibu, Ofisa Habari na Katibu Muhtasi, lakini Simba SC wametenga ‘kachumba kamoja’ wanabanana wote humo, Evodius Mtawala, Ezekiel Kamwaga, Matali na wote katika watendaji wa klabu.
  Hatukustaajabu Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele, ambaye kwa sasa ni Balozi wa FIFA alipozuru nchini alipelekwa Chamazi, yalipo makao makuu ya Azam, kwa Simba na Yanga SC pamoja na kuwa klabu kongwe, hazina sehemu ya kufikishia wageni.
  Simba SC na Yanga zinaweza kukosa vyote, lakini si angalau ofisi za maana na kumbi za mikutano zenye hadhi. Ila, katika kuendesha mambo kisasa tu, angalau Simba wanaipiga bao Yanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HAPA NDIPO SIMBA HUWA WANAJICHUKULIA 'POINTI ZA CHEE' DHIDI YA YANGA SC... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top