• HABARI MPYA

    Friday, May 24, 2013

    RAIS KIKWETE AFICHUA KWA NINI HAENDI UWANJA WA TAIFA KUANGALIA MECHI SIKU HIZI

    Rais Kikwete akizungumza na wachezaji wa Taifa Stars Ikulu jana Dar es Salaam
    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 24, 2013 SAA 6:30 MCHANA
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kwa sasa haendi Uwanja wa Taifa, wakati wa mechi za timu ya taifa, Taifa Stars kwa sababu amekwishakamilisha jukumu lake la kuwahamasisha wananchi kuipenda timu yao hiyo ya taifa.
    Akizungumza Ikulu mjini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema kwamba zamani alikuwa anakwenda sana katika mechi za timu hiyo, kwa sababu alikuwa anawahamasisha wapenzi wa soka nchini kuipenda timu yao na anashukuru hivi sasa wamekuwa wakimiminika kwa wingi kuishangilia timu hiyo.
    Kikwete alisema japokuwa haendi Uwanja wa Taifa, lakini hufuatilia mechi za timu hiyo kupitia Televisheni na amekuwa akiumia mno inapofanya vibaya.
    “Katikati hapa mambo yalivurugika, timu ikawa inafanya vibaya, lakini tangu bwana Kim (Poulsen) amekuwa kocha, timu imeanza tena kufanya vizuri, imeshinda mbili na tunafarijika sana,”alisema.
    Rais Kikwete alisema kwamba amefarijika sana na matokeo ya sasa ya timu hiyo, chini ya Kocha Mdenmark, Kim Poulsen na akawataka kuongeza juhudi kuhakikisha wanamaliza wakiwa wanaongoza Kundi C katika kampeni za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani Brazil.
    Amesema iwapo watafanya hivyo, atawafanyia kitu kizuri ambacho kitakuwa kumbukumbu nzuri katika maisha yao ya soka hata wakistaafu.
    Rais Kikwete amesema kwamba huwa anaumia sana timu hiyo inapofanya vibaya, kiasi cha kukosa hata raha mbele ya viongozi wenzake wa nchi nyingine wanaofuatilia soka anapokutana nao na kumuuliza matokeo ya Taifa Stars.
    “Wakati fulani mlifungwa na Msumbiji mechi ilichezwa usiku, mimi nilikuwa Arusha kwenye mkutano na Marais wenzangu, asubuhi yake wakaniuliza vipi matokeo ya mechi ya jana, kwa kweli nilikosa raha, niliwajibu hatukucheza vizuri sana na tulifungwa,”alisema.
    Rais Kikwete alisema anajua mchezo unaofuata dhidi ya Morocco Juni 8, mwaka huu mjini Marakech utakuwa mgumu kwa Stars, kwa sababu mechi iliyopita Tanzania iliifunga timu hiyo mabao 3-0 Dar es Salaam.
    “Lazima watakuwa wagumu kufungwa tena, najua utakuwa mchezo mgumu, lakini kajitahidini muwafunge tena, ili mradi kwanza mmalize mnaongoza hili Kundi, halafu mtaona tumewaandalia nini,”alisema. 
    Rais pia alimpongeza Kocha Poulsen kwa kuifikisha Stars sehemu nzuri na akamtaka kuongeza bidii kuhakikisha anaendeleza wimbi la ushindi, kwani timu ikianza kufanya vibaya hali itakuwa mbaya.
    Rais pia aliipongeza Kamati ya Saidia Stars Ishinde, ambayo mwanzoni mwa wiki iliwapa Sh. Milioni 30 wachezaji wa timu hiyo kama hamasa ili wafanye vizuri.
    Rais aliisifu Kamati hiyo kwamba inaundwa na watu ambao wanaijua soka, hivyo shaka itafanya kazi yake vizuri.
    Rais Kikwete aliwaalika wachezaji wa Stars chakula cha mchana Ikulu mjini Dar es Salaam jana.
    Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC, hakuwepo Ikulu jana kutokana na kufiwa na baba yake mlezi usiku wa jana, wakati Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wataungana na timu Marakech kutoka DRC, wanakochezea TP Mazembe.
    Wachezaji waliokuwapo Ikulu jana ni makipa; Nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).
    Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Mudathiri Yahya (Azam).
    Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
    Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, imeweka kambi katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambayo itatanguliwa na mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Sudan, Nile Crocodiles Juni 2 mwaka huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
    Hadi sasa, Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza tatu kushinda mbili na kufungwa moja, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, iliyoshinda mechi mbili na kutoa sare moja.
    Kama Stars itashinda ugenini dhidi ya Morocco, itajiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Brazil, kwani ikiongoza Kundi hilo, itacheza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini dhidi ya moja ya timu zilizoongoza makundi ambayo ikishinda itaweka historia ya kucheza Fainali za Kwanza za Kombe la Dunia.
    Stars, imekuwa na mwenendo mzuri chini ya Mdenmark Kim Pouslen, ambaye ameiwezesha kushinda mechi  tano kati ya 10, sare tatu na kufungwa mbili tangu aanze kazi Mei mwaka jana, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
    Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1, mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.
    Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAIS KIKWETE AFICHUA KWA NINI HAENDI UWANJA WA TAIFA KUANGALIA MECHI SIKU HIZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top