• HABARI MPYA

    Tuesday, May 28, 2013

    STARS WAANZA KUIPASHIA MOROCCO ADDIS

    Baadhi ya wachezaji wa Stars walio
    Addis Ababa, Zahor Pazi kulia
    na Mrisho Ngassa kushoto

    Na Boniface Wambura, Addis Ababa, IMEWEKWA MEI 28, 2013 SAA 10:30 JIONI
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetua mjini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya Shirika la Usafiri wa Anga la Misri ambako itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco, Simba wa Atlas itakayochezwa Juni 8 mwaka huu mjini Marrakech.
    Stars iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis.
    Kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Sudan, Mamba wa Mto Nile. Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis.
    Sudan ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0.
    Wachezaji wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.
    Kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3 mwaka huu kwa ndege ya Shirika la Usafiri wa Anga la Misri. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STARS WAANZA KUIPASHIA MOROCCO ADDIS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top