• HABARI MPYA

    Wednesday, May 29, 2013

    HUU NDIYO WASIWASI WANGU MKUBWA JUU YA KING KIBADEN NA SIMBA SC


    IMEWEKWA MEI 29, 2013 SAA 11:25 ALFAJIRI
    KUNA kitu kimoja ambacho kinanitatiza kwa muda mrefu, Watanzania hatujui kujivunia vitu vyetu na wakati mwingine, utamaduni huu unaingia hata katika maisha yetu binafsi. Mtu anaona kitu cha mwenzake ni bora kuliko cha kwake.
    Lakini ukweli ni kwamba, japo si kwa kiwango kikubwa, Watanzania wana mengi ya kujivunia, hususan katika mchezo wa soka. Siku moja nilikuwa najadili na kiongozi mmoja wa zamani wa Simba SC, Evans Aveva kama huyu Sunday Manara angetokea Kenya angekuwa na heshima kubwa kiasi gani.

    Mwaka jana nilikuwa Uganda katika michuano ya Kombe la CECAFA Challenge, mzee mmoja aliyejua mimi nimetokea Tanzania aliniuliza; “Yuko wapi Kibadeni”. Nilimtazama mara mbili yule mzee, tena kwa jicho la udadisi, kisha nikamjibu yuko Tanzania.
    Baada ya hapo, mzee huyo alianza kunielezea sifa za King Kibadeni enzi zake katika soka ya Afrika Mashariki na Kati, kwamba miaka ya 1970 yanapowadia mashindano ya CECAFA, iwe  Klabu Bingwa au Challenge Kibadeni alikuwa mmoja wa wachezaji wanaotia homa kubwa.
    Alimsifu sana, alikuwa ana uwezo mkubwa. Huyo Mganda anamsifu na kumtukuza Mtanzania. Je, hapa nyumbani ni makala ngapi zinaandikwa kuelezea wasifu wa Kibadeni? Binafsi, nikiwa gazeti la Dimba kati ya 1998 hadi 2012 nilipong’atuka, niliwaandikia makala wachezaji wengi waliowika kuanzia miaka ya 1960, Kibadeni alikuwa miongoni mwao.
    Hivyo ndivyo nilivyo, nathamini, naheshimu na kujivunia vya Tanzania. Ukweli ni kwamba, Waandishi wa Habari tunakabiliwa na changamoto ya kuihamaisha jamii kujivunia mashujaa wetu wa enzi hizo na hata wa leo pia na tusikubali sana kutekwa na Ulaya. Magazeti yetu ya michezo siku hizi, asilimia 70 ni habari za Ulaya, je kizazi kijacho kweli kitajua kulikuwa kuna mtu anaitwa Madaraka Selemani au Sanifu Lazaro? Sina hakika.  
    Hiyo si mada yangu leo, bali ni dibaji tu. Leo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ anatarajiwa kusaini Mkataba wa kuifundisha Simba SC kwa mwaka mmoja, akirithi mikoba ya Mfaransa, Patrick Liewig. Kibadeni atakuwa kocha wa kwanza mzawa kuifundisha Simba SC tangu mwaka 2000, Syllersaid Salmin Kahema Mziray (sasa marehemu) alipokuwa kocha wa mwisho mzawa Msimbazi.
    Katika msimu wa 2000, Simba ilipitia mikononi mwa makocha watatu, kwanza Mrundi Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’, baadaye Kibadeni na mwishoni, Mziray akaiongoza timu katika Kombe la FA, ikawa bingwa na kupata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza, tangu mwaka 1997, Kombe la Washindi.
    Baada ya hapo, Simba SC ikakabidhiwa kwa kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a na tangu hapo imekuwa ikifundishwa na makocha wa kigeni tupu. Imekuwa ikitokea mara chache katika kipindi chote hicho, tena kwa muda mfupi tu mzawa akapewa kazi ya kuifundisha Simba baada ya mgeni kuondoka.   
    Kwa mfano, marehemu Mziray mwaka 2008 aliombwa kumsaidia Mbulgaria Krasimir Bezinski, mwaka 2007, Talib Hilal ambaye kwa sasa ni raia wa Oman aliishika timu katika Ligi ndogo baada ya kuondoka Mbrazil, Neider dos Santos na Jamhuri Kihwelo mara kadhaa amekuwa akiishika timu hiyo, unapotokea udhuru wa makocha wa kigeni.
    Makocha waliopita Simba tangu 1998, kabla ya Kibadeni ni; Mfaransa Patrick Liewig (2013), Mserbia Milovan Cirkovick (2012), Mganda Moses Basena (2012), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Mzambia Patrick Phiri (2010), Mserbia Milovan Cirkovick (2009), Talib Hilal (2007), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Mzambia Patrick Phiri (2005), Mkenya James Siang’a (2001- 2004), Syllersaid Mziray (marehemu, 2000), Abdallah Kibadeni (2000), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (marehemu, 1999-2000), David Mwamwaja (marehemu, 1999), Mohamed Kajole (marehemu, 1998).
    Unaweza kuona kwa muda mrefu Simba SC ilipoteza imani na makocha wazawa, lakini ukijiuliza sababu huwezi kuipata, kwani makocha wazalendo wana rekodi nzuri ya mafanikio ndani ya klabu hiyo kuanzia marehemu Paul West Giwavaha aliyewafikisha Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na Kibadeni mwenyewe aliyewafikisha Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.
    Tunarudi kule kule, kutothamini vya kwetu ndio kunatuponza kuachana na walimu wetu wa hapa, wazuri na wa gharama nafuu na kubabaikia makocha wa kigeni, ambao wanalipwa fedha nyingi na kuzitia klabu gharama nyingine za ziada kama kuwalipia vibali vya kuishi nchini na kadhalika.
    Si vibaya kuwa na makocha wa kigeni, lakini tunapoamua kuwapa majukumu makocha wazawa, basi tukumbuke kuwajengea uwezo na mazingira ya kufanya kazi, kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa makocha wa kigeni.
    Leo Kibadeni anasaini Mkataba- sijui atalipwa kiasi gani mshahara kwa mwezi, wakati kocha aliyemtangulia, Liewig alikuwa analipwa Sh. Milioni 6 kwa mwezi, alipewa gari ya kutembelea, posho ya simu na alikuwa anaishi hoteli huku akitafutiwa nyumba ya kuishi, ingawa hilo halikutimia kwa sababu ameondolewa mapema tu (mwezi huu) tangu aanze kazi Januari. 
    Sahau kuhusu hayo yote, Kibadeni atapewa heshima sawa na Liweig kwa kutoingiliwa katika maamuzi na kuungwa mkono na uongozi?
    Liewig aliwaengua wachezaji nyota Simba SC akina Haruna Moshi ‘Boban’, Ramadhani Chombo Redondo, Amir Maftah, Paul Ngalema, Juma Nyosso kwa sababu za utovu wa nidhamu na akaamu kubaki na yosso watupu- lakini uongozi haukupingana naye.
    Najiuliza, akiwa kazini Kibadeni msimu ujao akagundua kuna wachezaji nyota wa uzito huo ni tatizo katika timu na akaamua kuwasimamisha, uongozi utamuelewa? Najiuliza hivyo kwa sababu nakumbuka mara ya mwisho Kibadeni aliondolewa Simba kwa sababu gani.
    Aligundua wachezaji wengi si waadilifu na alipotaka kupambana nao, uongozi wa wakati huo chini ya Mwenyekiti Abdul Yussuf Hazali ukamuondoa, vipi leo uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage utamuhesimu Kibadeni na kumpa fursa nzuri ya kufanya kazi?  
    Sahau kuhusu hayo, vipi kuhusu mazingira ya kufanyia kazi na vitendea kazi, Kibadeni atafanyiwa kama walivyokuwa wanafanyiwa wageni? Amini nakuambia, iwapo Simba SC itamchukulia Kibadeni kama mtaalamu na kuheshimu taaluma yake na majukumu yake, kisha wakamuwezesha na kumuunga mkono, anaweza kuvuka hata mafanikio aliyofikia na klabu hiyo mwaka 1993. Tatizo ni kwamba, Watanzania hatuthamini vya kwetu na haitakuwa ajabu Kibadeni akajutia kuondoka Kagera Sugar na kuja Simba SC. 
    Ila kwa nini Simba SC wasionyeshe mfano sasa kwa kumtengenezea mazingira mazuri Kibadeni na afurahie kazi Msimbazi? Kwa leo waungwana. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HUU NDIYO WASIWASI WANGU MKUBWA JUU YA KING KIBADEN NA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top