• HABARI MPYA

    Monday, May 20, 2013

    PILIKA ZA USAJILI ZAANZA, NGASSA AREJEA RASMI YANGA SC, SIMBA SC WAMTENGEA MILIONI 70 NIYONZIMA KULIPA KISASI JANGWANI...NA KAPOMBE NAYE...

    Amerudi nyumbani; Mrisho Ngassa na mashabiki wa Yanga waliomvalisja jezi Jumamosi

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 20, 2013 SAA 12:05 ASUBUHI
    BAADA ya kumalizika msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, vuguvugu la usajili limeanza rasmi na Mrisho Khalfan Ngassa anakuwa mchezaji wa kwanza kuhama klabu, akitoka Simba SC alikokuwa akicheza kwa mkopo na kurejea Yanga SC aliyowahi kuichezea kabla.
    Ngassa amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga SC na wakati wowote klabu yake mpya itamtambulisha rasmi kama amerejea nyumbani, baada ya kutoweka kwa miaka mitatu tangu 2010.
    Wakati Ngassa akiwa anarejea Jangwani, habari zaidi zinasema kwamba Simba SC nayo imepanga kujibu mapigo kwa kumsajili kiungo wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kwa dau la Sh. Milioni 70 walizokubaliana kwa mkataba wa miaka miwili.
    Anaondoka? Niyonzima anatakiwa Simba

    Simba SC pia wana wasiwasi, beki wao Shomary Kapombe anayemaliza mkataba wake Desemba mwaka huu akahamia Yanga SC.
    Kuhusu Ngassa, Simba SC imeamua kuachana  naye arejee Jangwani, lakini kwa Kapombe inapambana asing’oke kwa kuwa ina mipango naye mizuri.
    Kupitia Simba SC, tayari Kapombe ana ofa za majaribio Sunderland ya England na Uholanzi ambao kote anatakiwa kwenda kuanzia mwezi ujao.    
    Ngassa aliichezea Simba SC mechi ya 27 na ya mwisho Jumamosi katika kipindi cha kuwa kazini Msimbazi, wakati ilala mabao 2-0 mbele ya Yanga.
    Siku hiyo, Ngassa aliwajibika vizuri akiisaidia Simba SC kupata penalti dakika ya 27, baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, wakati huo Yanga inaongoza 1-0, lakini Mussa Mudde akapoteza nafasi ya kuisawazishia timu yake kwa mkwaju wake kuokolewa na Ally Mustafa ‘Barthez’.
    Katika mechi 27 alizoichezea Simba SC, zikiwemo za Ligi ya Mabingwa mbili, kirafiki kadhaa na Ligi Kuu, Ngassa amefunga jumla ya mabao saba na kutoa pasi za mabao 13.
    Baada ya mechi dhidi ya Yanga Jumamosi, mashabiki wa timu ya Jangwani walimfuata Ngassa na kumvalisha jezi ya timu hiyo, jambo ambalo liliwakera mashabiki wa Simba SC.
    Ngassa alitua Simba SC kwa mkopo Agosti mwaka jana akitokea Azam FC ya Dar es Salaam pia, ambayo nayo iliamua kumtoa kundini baada ya kukerwa na ‘Uyanga wake’.
    Ngassa alifunga bao la pili na la ushindi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika za lala salama katika Nusu Fainali ya Kombe la Kagame Uwanja Taifa, Dar es Salaam na kwenda kushangilia kwa kuibusu jezi ya Yanga, jambo ambalo liliwakera Azam na wakatangaza kumuuza.
    Hata hivyo, Simba SC ilifanikiwa kuipiku Yanga SC kwa kuuziwa mchezaji huyo kwa Sh. Milioni 25 kwa mkopo. Lakini alipotua Simba SC, ikaelezwa aliongeza mkataba wa mwaka mmoja na kupewa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 fedha taslimu na Milioni 18, thamani ya gari aina ya Verosa.  
    Lakini Ngassa mwenyewe alisema alipewa Milioni hizo 30 ili akubali kushuka Msimbazi na si kusaini mkataba mpya. 
    Ngassa alisajiliwa Azam Mei 21, mwaka 2010, kwa dola za Kimarekani 40,000, zaidi ya Sh. Milioni 60 kutoka Yanga SC, huku yeye mwenyewe akipewa dola 30,000, zaidi ya Sh. Milioni 45. 
    Alitua Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2006, akitokea Kagera Sugar ya Bukoba, ambayo ilimtoa Toto African ya Mwanza.
    Aprili mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio katika klabu ya West Ham United ya England wakati huo ipo chini ya kocha Mtaliano, Gianfranco Zola, ambako pamoja na kuvutia lakini akaambiwa ‘lishe ndogo’.
    Aliwahi pia kufanya majaribio Seattle Sounders FC ya Marekani na akapewa nafasi ya kucheza kwa dakika nane akitokea benchi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Manchester United na siku hiyo alikaribia kufunga pamoja na kumuumiza beki Rio Ferdinand. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: PILIKA ZA USAJILI ZAANZA, NGASSA AREJEA RASMI YANGA SC, SIMBA SC WAMTENGEA MILIONI 70 NIYONZIMA KULIPA KISASI JANGWANI...NA KAPOMBE NAYE... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top