• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 26, 2013

  DAU LA KIIZA LAIHENYESHA YANGA SC, KIPA NA MABEKI WAWILI HATARINI KUTEMWA JANGWANI

  Anaondoka? Hamisi Kiiza amewatajia dau ambalo Yanga hawako tayari kumpa

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 26, 2013 SAA 5:30 ASUBUHI
  MUSTAKABALI wa mshambuliaji Hamisi Friday Kiiza katika klabu ya Yanga upo shakani, kufuatia nyota huyo wa Uganda kushindwa kufikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo juu ya mkataba mpya.
  Vipengele vitatu vilijadiliwa mezani katika hoteli ya Protea mjini Dar es Salaam juzi, ambavyo ni mshahara, nyumba ya kuishi, gari na dau la kusaini mkataba mpya, lakini mwisho wa kikao haukuwa mzuri.
  Maombi mawili tu ya Kiiza yalikubaliwa na viongozi wa Yanga ambayo ni suala la nyumba na gari, lakini mshahara na dau la kusaini mkataba, pande hizo mbili, mchezaji na uongozi zilipingana.
  Kiiza alikubali kuondoka Yanga baada ya kushindwa kufikia makubaliano na uongozi, lakini baadaye jana akiwa anajiandaa kuondoka nchini kurejea Uganda, akapigiwa tena simu na viongozi kwa ajili ya mazungumzo zaidi.
  Hata hivyo, mfungaji huyo wa bao la pili la Yanga katika ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC Mei 18, mwaka huu alisema hawezi kupata muda wa mazungumzo zaidi, kwa kuwa anarejea haraka Uganda kujiunga na timu ya taifa chini ya kocha mpya, Milutin Sredojevic ‘Micho’.
  Uongozi ulimuomba kusogeza mbele safari yake japo kwa siku mbili ili upate muda wa kuzungumza naye tena mwishoni mwa wiki, lakini akasistiza hawezi na anarejea Uganda kuitikia wito wa timu ya taifa.
  Wakati hali ikiwa hivyo kwa Kiiza, kipa Said Mohamed na mabeki Godfrey Taita na Stefano Mwasyika nao pia wanachungulia mlango wa kutokea.
  Wachezaji hao wote watatu wamemaliza mikataba yao na ripoti ya kocha Ernie Brandts haijaonyesha umuhimu wao klabuni. Tayari kocha Brandts ameagiza asajiliwe kipa  mwingine na uongozi umeamua kumrejesha Mghana Yaw Berko.
  Hata hivyo, inadaiwa katika ripoti ya kocha Brandts amependekeza kiungo Kabange Twite asajiliwe, lakini uongozi kwa sasa unasaka mshambuliaji wa nguvu wa kigeni. 
  Maana yake, nafasi ya pacha huyo wa beki mwingine wa Yanga, Mbuyu Twite itakuwa finyu, kwa sababu tayari pamoja na Kiiza, klabu itakuwa na wageni wanne, kwani wapo pia Mbuyu, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na Didier Kavumbangu kutoka Burundi.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DAU LA KIIZA LAIHENYESHA YANGA SC, KIPA NA MABEKI WAWILI HATARINI KUTEMWA JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top