• HABARI MPYA

  Jumatano, Mei 22, 2013

  HAMISI KIIZA DIEGO KUSAINI MKATABA MPYA YANGA SC, ASEMA JANGWANI NI NYUMBANI SASA

  Anabaki;Kiiza akiwa amebeba Kombe la Bara Mei 18, mwaka huu kwa pamoja na mchezaji mwenzake, Simon Msuva kushoto

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 22, 2013 SAA 12:30 JIONI
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ amesema anatumai ataongeza mkataba Yanga baada ya ule wa awali wa miaka miwili kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, mfungaji huyo wa bao la pili katika ushindi wa 2-0 kwa Yanga dhidi ya mahasimu wao, Simba SC, Mei 18, mwaka huu, alisema kwamba amefanya mazungumzo na uongozi na ni matumaini atabaki.
  “Nitabaki, tumezungumza vizuri na uongozi. Na kwa kweli nafurahia maisha Yanga, kadiri ninavyozidi kuwa hapa (Tanzania) nazidi kuzoea na kupendezewa na hali ya hapa,”.
  “Nina imani kubwa tutafikia mwafaka na uongozi na kuongeza mkataba. Yanga ni sehemu ambayo nahisi kama nipo nyumbani, mashabiki wananikubali, wananifurahia na wananihamisha kufanya vizuri,”alisema.
  Kiiza alijiunga na Yanga Juni mwaka 2011 akitokea SC Villa ya Uganda, baada ya kung’ara na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya nchi hiyo na kuitoa Tanzania katika kinyang’anyiro cha kucheza Fainali za Michezo ya Afrika mwaka juzi nchini Msumbiji.
  Kiiza akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Bin Kleb



  Tangu atue Yanga, Kiiza ameiwezesha timu hiyo kushinda mataji matatu, mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame 2011 na 2012 na moja la Ligi Kuu ya Bara msimu huu.  
  Kiiza ni kati ya wachezaji wanne wa kigeni wa Yanga SC, wengine wakiwa ni beki Mbuyu Twite na kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na mshambuliaji, Didier Kavumbangu kutoka Burundi.  
  Amekuwa chini ya makocha wanne hadi sasa kuanzia Mganda mwenzake Sam Timbe aliyemkuta kazini, Mserbia Kosta Papic, Mbelgiji Tom Saintfiet na wa sasa Mholanzi, Ernie Brandts lakini wote wamekuwa wakimkubali na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HAMISI KIIZA DIEGO KUSAINI MKATABA MPYA YANGA SC, ASEMA JANGWANI NI NYUMBANI SASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top