• HABARI MPYA

    Friday, May 24, 2013

    TFF YAWAANDALIA ‘DARASA’ LA USAJILI WA KISASA VIONGOZI SIMBA, YANGA NA AZAM FC

    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA MEI 24, 2013 SAA 1:55 MCHANA
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeandaa semina ya usajili kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System-TMS) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ajili ya msimu wa 2013/2014.
    Semina hiyo itafanyika kesho kwenye ofisi za TFF, zilizopo ndani ya Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kuanzia Saa 3:00 asubuhi ikishirikisha watu wawili kutoka kila klabu ambao ni TMS Manager, na ofisa mwingine wa klabu.
    Klabu za ligi hiyo zinazotakiwa kuhudhuria semina ya usajili ni Ashanti United, Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Oljoro JKT, Rhino Rangers, Ruvu Shooting, Simba, Tanzania Prisons na Yanga.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Bin Kleb kushoto akiwa na Mrisho Ngassa baada ya kumsajili. Kulia Mussa Katabaro, Mjumbe wa Kamati hiyo

    Katika hatua nyingine, mechi za kwanza za Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii, Kamati ya Mashindano ya TFF imesisitiza kuwa wasimamizi wa mechi za ligi hiyo ni wenyeviti wa mikoa wa vyama vya mikoa.
    Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Ramadhan Nassib ilikutana jana (Mei 23 mwaka huu) kupitia ripoti za Makamisaa kwa mechi za Raundi ya kwanza ya RCL iliyomalizika wikiendi ya Mei 18 na 19 mwaka huu.
    Kuhusu viwanja vinavyotumika kwa ligi hiyo, Kamati imesema vitaendelea kuwa vile vya makao makuu ya mikoa, na kwa vile vilivyokuwa vimeombwa vifanyiwe marekebisho ili viweze kukaguliwa kwa ajili ya RCL msimu ujao na pia imeitaka mikoa kuendelea kuboresha viwanja vinavyotumika sasa, lakini vina upungufu.
    Vilevile Kamati imebaini kuwa zimekuwepo pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji ambapo imesema haiwezi kujadili pingamizi hizo kwa vile mikoa yote haikuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu husika uliofanyika mikoani kama ilivyoagizwa na kuelekezwa na TFF.
    Hata hivyo, Kamati imeitaka mikoa ambayo klabu zao zimefanikiwa kuingia raundi ya pili kuwasilisha usajili huo haraka.
    Pia Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya klabu ambazo zimekata rufani kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji, na kusisitiza kilichowasilishwa ni pingamizi kwa vile kwa mujibu wa kanuni masuala ya uwanjani hayakatiwi rufani. Hivyo, Kamati imeshauri klabu zilizokata rufani zilirejeshewe ada zilizolipa kwa ajili hiyo.
    Makamisaa na waamuzi wanaosimamia mechi za RCL wamekumbushwa kuwa ili mchezaji aruhusiwe kucheza mechi ni lazima awe na leseni yake (kadi ya usajili), vinginevyo asiruhusiwe kucheza mechi husika.
    Mechi za RCL zinaendelea wikiendi hii ambapo zote zitachezwa Jumapili (Mei 26 mwaka huu) isipokuwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.
    Nayo mechi kati ya Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi iliyokuwa ichezwe Jumamosi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam sasa itachezwa Jumapili kwa vile siku hiyo uwanja huo utatumika kwa mazoezi ya Taifa Stars.
    Mechi nyingine za RCL zitakazochezwa Mei 26 mwaka huu ni Machava FC ya Kilimanjaro dhidi ya Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
    Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi.
    Nayo Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
    Timu zitakazofuzu kucheza Raundi ya Tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TFF YAWAANDALIA ‘DARASA’ LA USAJILI WA KISASA VIONGOZI SIMBA, YANGA NA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top