• HABARI MPYA

  Jumanne, Mei 21, 2013

  HANS POPPE: NGASSA KAWAINGIZA MKENGA YANGA, WATAKIONA CHA MOTO

  Yanga wameingia mkenge? Hans Poppe anasema Ngassa mchezaji halali wa Simba SC

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 21, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema pamoja na kusaini Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa bado ni mchezaji halali wa klabu yake na ana makataba wa mwaka mmoja zaidi, aliosaini Agosti mwaka jana.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini Dar es Salaam, Poppe alisema kwamba hawana tatizo na mchezaji huyo kuondoka, bali wanataka taratibu zifuatwe na kwamba tofauti na hivyo suala hilo watalifikisha mbali, ikibidi hadi FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa).
  Akifafanua, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba Simba SC ilizinunua haki zote za mchezaji huyo kutoka Azam ambazo zilikuwa zinahusu mwaka mmoja na baada ya hapo wakazungumza naye na kuongeza mwaka mmoja zaidi.
  “Ngassa alisaini Mkataba wa Simba, akaweka saini na dole gumba, tena na tukampa fedha nzuri tu, kwamba ataichezea Simba SC hadi 2014 Agosti. Na hatukufanya hivi kienyeji, tulizungumza na Azam FC, wenyewe juu ya kurefusha mkataba wake, wakatukubalia,”.
  “Unajua nimegundua kitu kimoja, Yanga wana matatizo ya kutojua kanuni, ndiyo maana mwaka jana walitumia wachezaji ambao wamesimamishwa wakakatwa pointi. Hili tatizo ni kubwa na lazima walipatie ufumbuzi,”. “Wachukue muda wao kujifunza sheria, kanuni na taratibu zinazotawala soka, vinginevyo wataendelea kuwa kichekesho. Eti wanasema sisi tulisaini mkataba ndani ya mkataba hiyo hairuhusiwi, yaaani wanakariri kariri tu. 
  “Iko hivi, klabu hairuhusiwi kusaini mkataba na mchezaji bila kuzungumza na klabu yake, labda awe amebakiza miezi sita kumaliza mkataba. Sisi hatukusaini mkataba na Ngassa kienyeji, tulizungumza na klabu yake kwanza (Azam FC) ikatukubalia, tukazungumza na mchezaji pia akakubali na akasaini,” alisema Poppe.
  Ameongeza kwamba wanaamini Ngassa ni mtu mzima na mwenye akili timamu na nakala za mikataba aliyosaini Simba SC tayari zipo TFF, hivyo wanasubiri wakati ufike wapambane na Yanga kwenye vyombo vya sheria, kwani hawataki malumbano.
  Ngassa ametambulishwa rasmi asubuhi ya jana makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
  Ngassa aliichezea Simba SC mechi ya 27 na ya mwisho Jumamosi katika kipindi cha kuwa kazini Msimbazi, wakati ilala mabao 2-0 mbele ya Yanga.
  Siku hiyo, Ngassa aliwajibika vizuri akiisaidia Simba SC kupata penalti dakika ya 27, baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, wakati huo Yanga inaongoza 1-0, lakini Mussa Mudde akapoteza nafasi ya kuisawazishia timu yake kwa mkwaju wake kuokolewa na Ally Mustafa ‘Barthez’.
  Katika mechi 27 alizoichezea Simba SC, zikiwemo za Ligi ya Mabingwa mbili, kirafiki kadhaa na Ligi Kuu, Ngassa amefunga jumla ya mabao saba na kutoa pasi za mabao 13.
  Baada ya mechi dhidi ya Yanga Jumamosi, mashabiki wa timu ya Jangwani walimfuata Ngassa na kumvalisha jezi ya timu hiyo, jambo ambalo liliwakera mashabiki wa Simba SC.
  Ngassa alitua Simba SC kwa mkopo Agosti mwaka jana akitokea Azam FC ya Dar es Salaam pia, ambayo nayo iliamua kumtoa kundini baada ya kukerwa na ‘Uyanga wake’.
  Ngassa alifunga bao la pili na la ushindi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika za lala salama katika Nusu Fainali ya Kombe la Kagame Uwanja Taifa, Dar es Salaam na kwenda kushangilia kwa kuibusu jezi ya Yanga, jambo ambalo liliwakera Azam na wakatangaza kumuuza.
  Hata hivyo, Simba SC ilifanikiwa kuipiku Yanga SC kwa kuuziwa mchezaji huyo kwa Sh. Milioni 25 kwa mkopo. Lakini alipotua Simba SC, ikaelezwa aliongeza mkataba wa mwaka mmoja na kupewa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 fedha taslimu na Milioni 18, thamani ya gari aina ya Verosa.  
  Lakini Ngassa mwenyewe alisema alipewa Milioni hizo 30 ili akubali kushuka Msimbazi na si kusaini mkataba mpya. 
  Ngassa alisajiliwa Azam Mei 21, mwaka 2010, kwa dola za Kimarekani 40,000, zaidi ya Sh. Milioni 60 kutoka Yanga SC, huku yeye mwenyewe akipewa dola 30,000, zaidi ya Sh. Milioni 45. 
  Alitua Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2006, akitokea Kagera Sugar ya Bukoba, ambayo ilimtoa Toto African ya Mwanza.
  Aprili mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio katika klabu ya West Ham United ya England wakati huo ipo chini ya kocha Mtaliano, Gianfranco Zola, ambako pamoja na kuvutia lakini akaambiwa ‘lishe ndogo’.
  Aliwahi pia kufanya majaribio Seattle Sounders FC ya Marekani na akapewa nafasi ya kucheza kwa dakika nane akitokea benchi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Manchester United na siku hiyo alikaribia kufunga pamoja na kumuumiza beki Rio Ferdinand. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HANS POPPE: NGASSA KAWAINGIZA MKENGA YANGA, WATAKIONA CHA MOTO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top