• HABARI MPYA

    Wednesday, April 03, 2013

    NIYONZIMA: AKILI YANGU KUIPA YANGA UBINGWA, NALALA, NATEMBEA NIKIWAZA ULAYA, NALIA NA MUNGU WANGU

    Zawadi; Haruna akipokea zawadi ya fedha kutoka kwa mashabiki wa Yanga

    KATIKA siku za karibuni, vyombo vya Habari nchini vimekuwa vikiandika mengi kuhusu kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhili Niyonzima- kubwa kuhusu mustakabali wake katika klabu ya Yanga- Fuatilia mahojiano haya baina ya mchezaji huyo na mwandishi Mahmoud Zubeiry ili kujua zaidi kuhusu nyota huyo mwenye kipaji cha hali ya juu cha soka.
    Haruna akimtoka mchezaji wa Mtibwa Sugar katika moja ya mechi za Ligi Kuu

    BIN ZUBEIRY: Salaam alaykum.
    HARUNA: Waalaykum salaam. Mambo vipi? 
    BIN ZUBEIRY: Safi, pole na matatizo ya kifamilia yaliyokukwamisha kuitumikia timu yako katika mechi iliyopita. 
    HARUNA: Asante, yameisha na nimerudi kazini namshukuru Mungu. 
    BIN ZUBEIRY: Hebu tuanze na hili leo, Rwanda haifanyi vizuri siku za karibuni, tatizo nini?
    HARUNA: Nadhani inaweza kuwa inasababishwa na timu kubadilika, timu ni mpya, haijazoeana, na hata mfumo pia wachezaji hawajauelewa.
    BIN ZUBEIRY: Vipi kocha uwezo wake kwa ujumla
    HARUNA: Mimi huwa sipendi kuzungumzia sana kazi ya kocha, ila kwa kweli kocha naye ni binadamu, mechi ngapi hizi ambazo hajashinda, maana yake hajafanya vizuri. Lazima naye ajiangalie pia, mfumo wake na falsafa zake kwa ujumla kama zinaisaidia timu
    BIN ZUBEIRY: Ipi nafasi yenu kwa sasa kuelekea Brazil (Kombe la Dunia 2014)
    HARUNA: Matokeo yetu si mazuri, tuna pointi moja baada ya mechi tatu, maana yake nafasi yetu ni ngumu.
    BIN ZUBEIRY: Unadhani Ligi ya nyumbani (Rwanda) kwa sasa na mfumo kwa ujumla unasaidia kupatikana wachezaji bora wa timu ya taifa?
    HARUNA: Ni kweli, ligi ya nyumbani imebadilika, sasa hivi wanacheza wachezaji wengi wa nyumbani pale pale, hiyo inaweza kuwa inchangia timu ya taifa isiwe nzuri, kwa sababu upinzani umepungua, wageni wanaleta changamoto ambayo inakosekana kwa sasa.
    BIN ZUBEIRY: Tukirudi katika klabu yako, mnaongoza ligi kwa sasa, lakini Azam ipo nyuma yenu kwa tofauti ya pointi sita, hii haiwapi presha?
    HARUNA: Binafsi nadhani haitupi presha, jambo la maana hapa ni kuelekeza akili yetu sehemu na kutilia mkazo. Hakuna presha, kwa sababu tukishinda mechi mbili tutakuwa na uhakika wa ubingwa.
    BIN ZUBEIRY: Umecheza dhidi ya Azam msimu huu mara tatu na mmeifunga kuanzia Kombe la Kagame na Ligi Kuu mara mbili, unaizungumziaje Azam siku hadi siku
    HARUNA: Kwa kweli Azam imeimarika sana, ni haswa kwa maana ya timu, ina mipango, kwa ujumla wako vzuri, hata nafasi waliopo sasa ni nzuri ukilinganisha na mwaka jana.
    BIN ZUBEIRY: Vipi Yanga, inaimarika kutoka msimu umeanza tangu Kagame hadi sasa, ipo vile vile au inashuka?
    HARUNA: Mimi nawapongeza wachezaji wenzangu, mechi zote tunazocheza ni ngumu kama fainali, kila timu inataka iifunge Yanga iweke historia, haikuwa kazi rahisi kufika hapa tulipo, hatujamaliza vita, tuendelee kushikamana ili tutimize malengo yetu. Ila nawapongeza sana wachezaji wenzangu.
    BIN ZUBEIRY: Mlifungwa 5-0 na Simba mwaka jana, vipi mtalipa kisasi?
    HARUNA: Mimi kama mchezaji, matokeo yoyote yanatokea, ila hatuwezi kukubali kufungwa tena na Simba, itaonekana wao wanatuweza sana, sizungumzii idadi ya mabao, cha muhimu ni pointi tatu, mabao matano ni vizuri tukirudisha.
    BIN ZUBEIRY: Kwa uzoefu wako, unadhani kwa nini mabao yamekuwa adimu Yanga kwa sasa tofauti na mwanzoni.
    HARUNA: Kwa kweli, cha kwanza ni kupata nafasi, lakini hatuzitumii ipasavyo, cha pili ni bahati mbaya, lakini pia wachezaji wa mbele wanatakiwa wawe makini. Na pia kila mechi watu wanatupania sana, sare ya Jumamosi na Polisi Morogoro si tatizo, ilikuwa ugenini, na Uwanja wa Morogoro. Mimi kama mimi nisingependa timu zichezee Morogoro, ni mbaya sana. Pamoja na hayo, katika kila mazoezi mwalimu anaongea sana, anatuambia umuhimu wa kutumia nafasi. Naamini tutajirekebisha.
    BIN ZUBEIRY: Ukipewa fursa ya kuchagua wachezaji wawili wa kusajili Yanga kutoka timu nyingine za hapa Bara, utawachua akina nani
    HARUNA: Kwanza ni  Mwinyi Kazimoto  (wa Simba SC) na pili Emanuel Swita (wa Toto Africans).
    BIN ZUBEIRY: Kwa nini hao
    HARUNA: Kwa sababu mimi huwa ninapenda sana wachezaji wanaocheza kwa kutumia akili, Mwinyi na Sita na wana uwezo mkubwa na wanatumia akili sana uwanjani. 
    BIN ZUBEIRY: Ukiwa na umri wa miaka 25 sasa, bado una matarajio ya kucheza Ulaya?
    HARUNA: Yapo, lakini katika maisha unatakiwa kuwa na bahati pia, nikilala nikiamka, nikitembea nawaza kucheza Ulaya, hadi nasali namuomba Mungu anijaalie nicheze Ulaya siku moja, naomba japo kwa mwaka mmoja tu nicheze Ulaya na ninajua nitafanya kitu. Ulaya nimekwishafika na nimekwishaona wanachezaje, naamini ninaweza.
    BIN ZUBEIRY: Mkataba wako Yanga unaisha lini…
    HARUNA: Mkataba wangu ulikuwa wa miaka miwili, unaisha sasa, lakini akili yangu ipo kwenye kuipatia timu yangu ubingwa…baada ya hapo ndio nitajua masuala ya mkataba.
    BIN ZUBEIRY: Ukipata ofa nzuri kutoka timu nyingine hapa mfano Azam, Simba SC unaweza kuhama Yanga?
    HARUNA: Nitakuwa tayari kuondoka, ikiwa katika mazungumzo yangu na Yanga juu ya mkataba mpya hatutakubaliana. Mimi ni mchezaji, naangalia maisha yangu ya baadaye, nataka nikistaafu, watoto wangu waishi vizuri na mimi pia niishi vizuri, hivyo lazima niweke maslahi mbele.
    BIN ZUBEIRY: Nini falsafa yako katika soka?
    HARUNA: Falsafa yangu ni mapenzi na timu nayaoichezea, nacheza kwa uadilifu na mapenzi. Hiyo ni falsafa yangu tangu nipo Rayon na APR kule nyumbani (Rwanda). Na hata hapa Yanga unaweza kuona, nacheza kama timu ya baba yangu. Lakini popote nitakapokwenda itakuwa hivyo.
    BIN ZUBEIRY: Nafikiri kwa leo inatosha Haruna. Nashukuru sana kwa ushirikiano na nikutakie kila la heri katika maisha yako.
    HARUNA: Asante sana, kazi njema na karibu tena BIN ZUBEIRY.
    Haruna akitafuta mbinu za kuwatoka Kipre Tchetche na Kipre Balou wa Azam FC
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NIYONZIMA: AKILI YANGU KUIPA YANGA UBINGWA, NALALA, NATEMBEA NIKIWAZA ULAYA, NALIA NA MUNGU WANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top