• HABARI MPYA

    Thursday, April 04, 2013

    KIPA BORA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA 2012/2013 NI VITA YA KASEJA, BARTHEZ NA WENGINE WAWILI


    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaelekea ukingoni, tayari mataji mawili yana mwelekeo ya kwenda sehemu fulani.
    Ubingwa wenyewe wa Ligi Kuu umekaa katika mwelekeo wa kwenda Jangwani, yalipo maskani ya Yanga SC ambao wanaongoza ligi hiyo kwa wastani wa pointi sita zaidi.
    Tuzo ya ufungaji bora ipo kwenye mwelekeo wa kwenda Chamazi, yalipo maskani ya Azam FC kwa mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche.
    Lakini kitendawili kigumu ni nani atakuwa kipa bora wa Ligi Kuu msimu huu wa 2012/2013?
    Makipa wanne wanapewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo hiyo kutokana na kuziongoza vyema timu zao licha ya changamoto za hapa na pale.
    Hao ni Juma Kaseja wa Simba SC anayeshikilia tuzo hiyo, Ally Mustafa ‘Barthez’ wa Yanga, Mwadini Ally wa Azam FC na Hussein Sharrif ‘Cassillas’ wa Mtibwa Sugar.

    JUMA KASEJA:
    Alikosa mechi moja tu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, dhidi ya Toto African na katika mzunguko huu wa pili, pia hadi sasa amekosa mechi moja tu dhidi ya Coastal Union, zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa kuwa Kaseja ameendelea kuwa kipa chaguo la kwanza timu ya taifa, Taifa Stars, maana yake anafanya kazi nzuri Simba SC.
    Kweli, Simba haipo kwenye nafasi nzuri katika Ligi Kuu hivi sasa, lakini hiyo inasababishwa na matatizo ya timu kwa ujumla, ila bado unaweza kukubali Kaseja anafanya kazi yake vizuri.
    Akiwa anashikilia tuzo hiyo, dhahiri Kaseja anakabiliwa na changamoto ya kuitetea dhidi ya makipa wengine wanaofanya vizuri kwa sasa nchini akina Mwadini Ally wa Azam, Ally Mustafa ‘Barthez’ wa Yanga na Hussein Sharrif ‘Cassilas’ wa Mtibwa Sugar.
    Juma Kaseja amedaka mpira wa juu dhidi ya Hussein Javu wa Mtibwa

    MWADINI ALLY:
    Angalau mzunguko wa kwanza wakati wa kocha Mserbia, Boris Bunjak Mwadini alikuwa anapokezana na Deo Munishi ‘Dida’ kudaka Azam.
    Lakini tangu kurejea Muingereza Stewart Hall mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Mwadini amekuwa kama alama ya lango la Azam, habanduki.
    Mzunguko huu wa pili, alikosa mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani na hiyo ni kwa sababu alikuwa majeruhi akasaidiwa na Aishi Manula.
    Mwadini ameendelea kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars, ingawa kama kipa wa akiba baada ya Kaseja. 
    Huyu ni miongoni mwa makipa wanaofanya kazi nzuri katika Ligi Kuu na wazi ataingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu msimu huu.
    Mwadini ameruka kupangua mpira wa juu huo unaelekea nje

    ALLY BARTHEZ:
    Mzunguko wa kwanza alikuwa anapokezana na Yaw Berko, lakini tangu kuanza kwa mzunguko huu wa pili amekuwa akidaka peke yake.
    Ameonyesha uwezo mkubwa wa kudaka hata katika mechi ngumu akiiwezesha Yanga kuondoka na pointi tatu.
    Ukweli ni kwamba, Barthez msimu huu amedhihirisha Simba SC ilikuwa haimtendei haki kumuweka benchi msimu mzima, miaka yote.
    Pamoja na uhodari wote, Barthez hajamvutia kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ambaye ameona bora kuita kipa wa benchi wa Azam, Aishi Manula kwenye kikosi chake kuliko Yanga One huyo. 
    Lakini hiyo haimzuii Barthez kuwa mmoja wa washindani wakuu wa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu msimu huu na wapinzani wake wazi watakuwa Juma Kaseja na Mwadini Ally. 
    Barthez amedaka mpira wa juu dhidi ya wachezaji wa Azam FC

    HUSSEIN CASSILLAS:  
    Katika mzunguko wa kwanza alikuwa anapokezana na Shaaban Kado kudaka katika lango la Mtibwa Sugar ya Morogoro, kijiji cha Lusanga, Manungu.
    Lakini tangu kuanza kwa mzunguko huu wa pili, Cassilas amekuwa akidaka mfululizo peke yake na kuonyesha umahiri wa hali ya juu.
    Dar es Salaam nzima sasa wanamjua Cassilas ni nani baada ya kudaka kwa uhodari mkubwa dhidi ya Simba na Yanga Uwanja wa Taifa. 
    Na haikuwa ajabu Cassilas akaitwa Taifa Stars baada ya kazi nzuri aliyoifanya Mtibwa Sugar na haitakuwa ajabu pia kipa huyo chipukizi kuingia kwenye orodha ya wanaowania tuzo ya kipa bora wa msimu.
    Cassilas ameruka kugombea mpira wa juu na wachezaji wa Yanga

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIPA BORA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA 2012/2013 NI VITA YA KASEJA, BARTHEZ NA WENGINE WAWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top