Yanga wamemaliza kileleni |
Na Mahmoud Zubeiry
MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
rasmi umemalizika jana ukiacha mechi mbili za viporo za Tanzania Prisons, dhidi
ya Mgambo JKT na Ruvu Shooting.
Prisons walipata ajali wakiwa njiani kuelekea Tanga kwa ajili
ya mechi yao na Mgambo JKT, hivyo mechi hiyo na ile iliyofuata dhidi ya Ruvu
Shooting zikaahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine, ili kuwapa wachezaji wake
nafasi ya kupona majeruhi.
Mzunguko wa kwanza umemalizika na matokeo yamekuwa tofauti na
mwelekeo wa ligi hiyo katika mzunguko huo, hadi katikati yake.
Yanga SC, ambayo haikutarajiwa kushika hata nafasi ya pili,
ndiyo imemaliza kileleni kwa pointi zake 29, baada ya mechi hizo 13, ikifuatiwa
na Azam FC yenye pointi 24 na Simba SC yenye pointi 23.
Presha ilikuwa upande wa mashabiki wa Yanga ndani ya mechi
tano za mzunguko wa kwanza, kutokana na kuanza vibaya, kiasi cha kufikia
kumfukuza kocha wake aliyewapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Saintfiet alifukuzwa baada ya mechi mbili za Ligi Kuu, akitoa
sare na Prisons mjini Mbeya na kufungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar mjini
Morogoro.
Azam nayo ilianza vema ikiwa nyuma ya Simba SC, lakini
ilifukuza kocha wake Mserbia Boris Bunjak baada ya kufungwa mabao 3-1 na Wekundu
hao wa Msimbazi.
Naam, Tanzania mechi moja au mbili za kufungwa zinatosha
kumfukuzisha kocha na watu sasa wanasubiri hatua itakayochukuliwa na Simba
dhidi ya kocha wake, Mserbia pia, Profesa Milovan Cirkovick baada ya klabu hiyo
kufungwa mechi mbili mfululizo, 2-0 na Mtibwa Sugar na 1-0 na Toto.
Tayari kundi la Friends Of Simba ambalo linasaidia sana
uendeshwaji wa klabu hiyo limeripotiwa kushinikiza Milovan afukuzwe na
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amesema Ijumaa wiki hii
atachukua maamuzi magumu. Tusubiri.
Lakini tumeshuhudia timu mpya iliyopanda Ligi Kuu msimu huu,
ambayo imeleta changamoto mpya, JKT Mgambo pamoja na kuimarika kwa Coastal
Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, ambazo zinatoa upinzani katika ligi hiyo
hata kwa vigogo.
Kwa kiasi kikubwa msimu huu tuna ligi tofauti na ya msimu
uliopita na kama timu zitafanya maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa mzunguko
wa pili, ni matarajio ya wengi Ligi Kuu itaisha vizuri zaidi.
Yanga SC 2012 |
YANGA SC:
Wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu,
wakiwa na pionti zao 26, baada ya kucheza mechi 13, kufungwa mbili dhidi ya
Mtibwa Sugar 3-0 na Kagera Sugar 1-0, zote ugenini, kutoa sare mbili 1-1 dhidi
ya Simba SC na 0-0 dhidi ya Prisons.
Yanga ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu Ligi Kuu,
ilipanda kileleni Novemba 4, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 na kuwashusha
mabingwa watetezi, walioongoza ligi hiyo tangu mwanzoni.
Katikati ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilifikia kuzidiwa
pointi saba na Simba lakini Oktoba 31, ikafanikiwa kuwafikia Wekundu hao wa
Msimbazi, siku hiyo wao wakiifunga Mgambo JKT 3-0 Dar es Salaam na wapinzani
wao wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro.
P W D L GF GA GD Pts
1 Yanga SC 13 9 2 2 25 10 15 29
KOCHA; Ernie
Brandts (Uholanzi)
Azam FC 2012 |
AZAM FC:
Imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi
ya pili, kwa pointi zake 24, ikiwazidi pointi moja tu mabingwa watetezi, Simba
SC. Azam walikuwa na mwelekeo wa kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kama si
kufungwa mechi mbili mfululizo za mzunguko wa kwanza, dhidi ya Yanga 2-0 na
Mgambo JKT 2-1.
Azam ilianza vema tu ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba tangu
mwanzo hadi Oktoba 31, ilipoenguliwa na Yanga katika nafasi ya pili. Ikielekea
kwenye mechi yake ya mwisho dhidi ya Mgambo, Azam ilifukuza wachezaji wake
wanne, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa madai
walipokea hongo waifungishe timu hiyo dhidi ya Simba na wanadai wana ushahidi
hadi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Dhahiri kuondolewa
kwa wachezaji hao tegemeo kikosini kulichangia matokeo ya kufungwa na Mgambo
katika mechi ya mwisho.
P W D L GF GA GD Pts
2 Azam FC 13 7 3 3 17 11 6 24
KOCHA: Stewart
Hall (Uingereza)
Simba SC 2012 |
SIMBA SC:
Mabingwa hao watetezi, waliianza Ligi Kuu vema wakionyesha
dalili zote za kutetea ubingwa wao kwa kufanikiwa kuwa kileleni hadi mwishoni
mwa mzunguko huo, kabla ya mambo kugeuka ghafla.
Zilianza sare kwanza, 1-1 na Yanga, 0-0 na Coastal Union, 2-2
na Kagera Sugar na baadaye 0-0 na Mgambo, 0-0 na Polisi Morogoro kabla ya
kufungwa mechi ya kwanza msimu huu, mbele ya Mtibwa Sugar na kumaliza mzunguko
wa kwanza kwa kipigo cha 1-0 kutoka kwa Toto Africans.
Matokeo haya kwa kiasi kikubwa yameivuruga Simba SC na
inasemekana Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
anafikiria kujiuzulu na baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar, hakujihusisha na
chochote juu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Toto, wakati huo Mwenyekiti wake,
Alhaj Ismail Aden Rage yuko bize na shughuli za kisiasa Dodoma. Rage anasema
amekwishawajua wanaosababisha matokeo mabaya Simba na Ijumaa atatangaza maamuzi
magumu.
P W D L GF GA GD Pts
3 Simba SC 13 6 5 2 20 11 9 23
KOCHA: Milovan
Cirkovick (Serbia)
Mtibwa Sugar 2012 |
MTIBWA
SUGAR:
Ilianza vizuri, katikati ikavurunda na mwishoni mwa mzunguko
wa kwanza ikazinduka tena hatimaye imemaliza katika nafasi ya nne kwenye
msimamo wa Ligi Kuu.
Inaonekana Mtibwa Sugar inaanza kurejesha makali yake
iliyoingia nayo katika soka ya Tanzania miaka ya 1990 hadi wakafanikiwa kutwaa
ubingwa wa ligi hiyo mara mbili mfululizo 1999 na 2000, wakiweka rekodi ya kuwa
timu pekee nje ya Simba na Yanga kutetea taji hilo.
Hiyo si kwa sababu tu ipo nyuma ya Yanga, Azam na Simba, bali
msimu huu imefanikiwa kuvifunga vigogo vyote vya soka nchini, Simba na
Yanga.
P W D L GF GA GD Pts
4 Mtibwa Sugar 13 6 4 3 18 12 6 22
KOCHA: Mecky
Mexime (Mzalendo)
Coastal Union 2012 |
COASTAL
UNION:
Wana Mangushi wamerudi tena kwenye makali yao yaliyowafanya
wakawa mabingwa wa ligi hiyo mwaka 1988, kwani hadi sasa wameonyesha upinzani
wa kutosha kwenye Ligi Kuu. Wagosi hao wa Kaya wamemaliza katika nafasi ya tano
kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 sawa na Mtibwa walio nafasi ya
nne, lakini wanazidiwa wastani tu wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, Coastal walianza Ligi Kuu kwa kusuasua kiasi cha
kufikia kuwafukuza makocha wake wa awali waliosajili na kuandaa timu kwa ajili
ya ligi hiyo, Juma Mgunda na Habib Kondo ambao nafasi zao zilichukuliwa na
Hemed Morcco na Ally Kiddy.
P W D L GF GA GD Pts
5 Coastal Union 13 6 4 3 16 14 2 22
KOCHA: Hemed Morocco
(Zanzibar)
Kagera Sugar 2012 |
KAGERA
SUGAR:
Kagera Sugar wamemaliza katika nafasi ya sita wakiwa na
pointi 21 na wangeweza kumaliza juu ya hapo, kama wangeutumia vizuri mchezo wao
wa mwisho kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
Wakipewa nafasi kubwa ya kushinda, katika mastaajabu ya
wengi, Kagera wakalazimishwa sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Morogoro
kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, hivyo kuwapa nafasi Coastal na Mtibwa
kuendelea kuwa juu yao.
Kagera inajivunia kutofungwa na vigogo wa soka nchini, kwani
waliifunga Yanga 1-0 na wakatoa sare ya 2-2 na Simba na Dar es Salaam.
P W D L GF GA GD Pts
6 Kagera Sugar 13 5 6 2 15 10 5 21
KOCHA: Abdallah
Athumani Seif ‘Kibadeni’ (Mzalendo)
Ruvu Shooting 2012 |
RUVU
SHOOTING:
Katika timu zote za majeshi kwenye ligi hiyo, Ruvu Shooting
ndio inaonekana kuwa imara zaidi na ndiyo maana ipo katika nafasi nzuri zaidi,
ikiwa imebakiza mechi moja ya kiporo dhidi ya Prisons kumaliza mechi zake za
mzunguko wa kwanza.
Ruvu ipo katikati ya msimamo wa ligi, nafasi ya saba kwa
pointi zake 17 na inaweza kumaliza na pointi 20 iwapo itaifunga Prisons, lakini
itaendelea kubaki kwenye nafasi hiyo hiyo, kwani Kagera Sugar waliopo juu ya
wana pointi 21.
Timu hii inayotumia Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani ni
moja kati ya timu zilizoonyesha kandanda safi ya kuvutia, tena ikiundwa na
wachezaji wengi chipukizi, kama Seif Abdallah anayegombea kiatu cha
dhahabu.
P W D L GF GA GD Pts
7 Ruvu Shooting 12 5 2 5 17 17 0 17
KOCHA: Charles
Boniface Mkwasa (Mzalendo)
JKT Ruvu 2012 |
JKT RUVU:
Imeshuhudiwa katika msimu mwingine, timu hii inazidi kupoteza
makali yake, baada ya kumaliza katika nafasi ya nane mzunguko wa kwanza wa Ligi
Kuu.
Siyo JKT ile ambayo ilikuwa tishio kwa vigogo, Simba na Yanga
bali hii ya sasa ni ‘urojo’ na hali hii inatokea huku ikiwa inaundwa karibu na
asilimia kubwa ya wachezaji wake wale wale, walioifanya iwe tishio misimu
michache iliyopita, tena wakiwa chini ya kocha yule yule, kiungo wa zamani wa
Yanga, Charles Killinda.
P W D L GF GA GD Pts
8 JKT Ruvu 13 4 3 6 13 20 -7 15
KOCHA: Charles
Kilinda (Mzalendo)
TZ Prisons 2012 |
TZ PRISONS:
Imerejea Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa unaweza kusema
inapambana kuhakikisha inabaki kwenye ligi hiyo msimu ujao. Prisons wana mechi
mbili za viporo dhidi ya Mgambo JKT na Ruvu Shooting ambazo zote watacheza ugenini,
lakini hadi sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Timu hiyo iliahirishiwa mechi zake baada ya kupata ajali, ikiwa inaelekea Tanga
kumenyana na Mgambo na wachezaji wake sita wakaumia. Inaweza kupanda juu
kiidogo iwapo itashinda mechi zake mbili zilizobaki.
P W D L GF GA GD Pts
9 Prisons 11 3 5 3 8 9 -1 14
KOCHA: Jumanne
Charles (Mzalendo)
JKT Oljoro 2012 |
JKT OLJORO:
Haina makali yake iliyoingia nayo kwenye Ligi Kuu msimu
uliopita yaliyowafanya wamalize mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni. Msimu huu
JKT Oljoro imemaliza katika nafasi ya 10 kwa pointi zake 24 na huwezi kusita
kusema ipo kwenye hatari ya kushuka daraja hadi sasa.
Ina pointi 14, sawa na Toto Africans iliyo nafasi ya 11 na
inabebwa juu kwa wastani wa bao moja tu katika mabao ya kufunga na kufungwa,
huku ikiwa inaizidi kwa pointi mbili tu Africans Lyon iliyo nafasi ya 12- JKT
Oljoro hakika imemaliza mzunguko wa kwanza katika eneo baya.
P W D L GF GA GD Pts
10 JKT Oljoro 13 3 5 5 13 16 -3 14
KOCHA: Mbwana
Makatta (Mzalendo)
Mgambo JKT 2012 |
MGAMBO JKT:
Ligi Kuu ya Bara imepokea timu mpya tushio ambayo imeongeza
ladha katika ligi hiyo. Hiyo si nyingine zaidi ya JKT Mgambo ua Handeni, Tanga
inayotumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga pamoja na Coastal Union. Ikiwa na mechi
moja ya kiporo mkononi dhidi ya Prisons, Mgambo ipo nafasi ya 11 kwa pointi
zake 14 na kama ikifanikiwa kushinda mchezo huo, inaweza kupanda hadi nafasi ya
saba, itategemea pia na matokeo ya mchezo mwingine wa kiporo kati ya Ruvu
Shooting na Prisons. Mgambo walianza kwa kusuasua na watu wakaitabiria itashuka
daraja, ila ilipokuja kuzinduka mwishoni mwa msimu, watu wamebadilisha kauli
zao.
P W D L GF GA GD Pts
11 Mgambo JKT 12 4 2 6 9 13 -4 14
KOCHA: Mohamed
Kampira (Mzalendo)
Toto Africans 2012 |
TOTO
AFRICANS:
Wana Kishamapanda bado wapo katika wakati mgumu, kwani
wamemaliza Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ndani ya nafasi tatu
za kushuka Daraja.
Washukuru sana ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye
mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, kwani umewainua kidogo, vinginevyo
wangemaliza ligi hiyo vibaya zaidi.
Lakini hii ni timu ambayo inacheza kwa ushindani zaidi
inapokutana na timu tishio, ila kwa timu ambao zinaonekana si tishio, Toto
hufanya vibaya. Bila shaka kuna kudharau mechi, ambako ndiko kunawaponza na
kama watabadilika mzunguko wa pili, wanaweza kmufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu.
P W D L GF GA GD Pts
12 Toto Africans 13 2 6 5 10 15 -5 12
KOCHA: John
Tegete (Mzalendo)
African Lyon 2012 |
AFRICAN
LYON:
Hali bado ni tete African Lyon, ikiwa imemaliza mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu katika nafasi ya 13 kwa pointi zalke tisa. Licha ya kunolewa
na kocha Muargentina, Pablo Ignacio Velez, lakini Lyon wamekuwa vibonde tu hadi
sasa.
Mmiliki wa timu hiyo, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amesema kwamba
ametenga dau la dola za Kimarekani 200,000 kwa ajili ya kufanya usajili dirisha
dogo ili kuimarisha kikosi na miongoni mwa wachezaji aliowalenga ni Emmanuel
Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba na Mbuyu Twite wa Yanga. Amesema kwa Twite
atatoa dola 100,000, Ngassa dola 40,000 na Okwi dola 60,000. Tusubiri, ila hadi
sasa hali tete Lyon.
P W D L GF GA GD Pts
13 African Lyon 13 2 3 8 9 20 -11 9
KOCHA: Pablo
Ignacio Velez (Argentina)
Polisi Morogoro 2012 |
POLISI
MOROGORO:
Imerejea Ligi Kuu msimu huu, lakini haitakuwa ajabu mwishoni
mwa msimu ikarudi tena kucheza Ligi Daraja la kwanza. Timu ya Morogoro,
imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inashika mkia. Polisi
haijashinda mechi hata moja zaidi ya kutoa sare nne na kufungwa mechi nyingine
tisa.
Sijui maajabu gani yatokee, msimu ujao tuendelee kuwa na timu
ya Morogoro, kwani kulingana na ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, hakuna dalili
za Polisi kupona.
P W D L GF GA GD Pts
14 Polisi Morogoro 13 0 4 9 4 16 -12 4
KOCHA: John
Simkoko (Mzalendo)