• HABARI MPYA

    Saturday, October 13, 2012

    BAHANUZI SPIDER MAN KUANZA MAZOEZI MEPESI JUMATATU, YONDAN HAKIJAELEWEKA

    Said Bahanuzi

    Na Mahmoud Zubeiry
    MSHAMBULIAJI wa Yanga, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi keshokutwa kufuatia kuchanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki hii.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Daktari wa Yanga, Sufiani Juma ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo kwamba, mfungaji huyo bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, anaendelea vizuri baada ya kuchanika nyama za paja la mguu wa kulia.
    Yondan alivyoumizwa na Boban
    “Lini haswa ataingia kwenye programu kamili ya mazoezi, itategemea na maendeleo yake atakapoanza mazoezi mepesi,”alisema Sufiani.
    Kuhusu beki Kevin Yondan aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kugongwa na Haruna Moshi ‘Boban’, Sufiani alisema naye anaendelea vizuri na wakati wowote wiki ijayo ataanza mazoezi mepesi.
    Zaidi ya hao, Sufiani alisema Yanga ina majeruhi mwingine mmoja tu, ambaye ni Salum Telela ambaye naye anaendelea vizuri.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Baada ya ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu mjini Mwanza, Yanga inatarajiwa kuendelea na mazoezi Jumatatu, kujiandaa na mechi ijayo, dhidi ya Ruvu Shooting Oktoba 20, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BAHANUZI SPIDER MAN KUANZA MAZOEZI MEPESI JUMATATU, YONDAN HAKIJAELEWEKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top