• HABARI MPYA

    Monday, October 01, 2012

    MTIBWA SUGAR WAPO CHAMAZI LEO LIGI KUU

    Mtibwa Sugar

    Na Princess Asia
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja tu utakaopigwa kwenye Uwanja Chamazi, Dar es Salaam, kati nya Ruvu Shooting ya Pwani na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi lakini kwa sababu ya kuonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini umehamishiwa Uwanja wa Azam.
    Unatarajiwa kuwa mchezo mzuri usio na jakamoyo na bila shaka watakaoushuhudia kupitia Super Sport watafurahia soka ya kuvutia. Mechi nyingine za ligi hiyo zilichezwa mwishoni mwa wiki, kuanzia Ijumaa na kurushwa pia moja kwa moja na Super Sport.
    Katika mchezo wa jana, Yanga ilishinda mabao 3-1 dhidi ya African Lyon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shukrani kwake kiungo anayecheza kwa nadra kwenye timu hiyo, Nizar Khalfan aliyefunga mabao ya ushindi dakika ya 65 na 88, akitokea benchi kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
    Nizar alifunga bao la pili, sekunde chache baada ya Benedictor Mwamlangala kuisawazishia African Lyon bao lililodumu tangu dakika ya 17, baada ya Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutangulia kufunga dakika ya 17.
    Ushindi huo, unaifanya Yanga ifikishe pointi saba, baada ya kucheza mechi nne na kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikiwa inalingana na Coastal kwa pointi na wastani wa mabao, ingawa Coastal wako nyuma kwa mechi moja.
    Simba iliichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.
    Simba bado inaongoza ligi hiyo, kwa pointi zake 12, ikifuatiwa na Azam iliyoifunga JKT Ruvu 3-0 Ijumaa, mabao ya John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Herma Tchetche na Kipre Michael Balou yenye pointi 10.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR WAPO CHAMAZI LEO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top