• HABARI MPYA

    Saturday, August 11, 2012

    SIMBA KUMSHITAKI KIGEUGEU MBUYU TWITE

    Hanspop
    KLABU ya Simba imesema itamfikisha mahakamani mchezaji Mbuyu Twite wa klabu ya APR kwa kosa la kuwatapeli na kukubali kusajiliwa na Yanga.
    Mwenyekiti wa kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope amekaririwa na liwazozito.blogspot.com akisema, Twite alishapokea fedha za Simba na kukubali kuingia nayo mkataba, hivyo hawezi kwenda kinyume.
    Hanspope alisema kilichofanywa na Yanga kumshawishi mchezaji huyo arejeshe fedha za Simba na kupokea fedha zao ni cha kihuni na hawawezi kukivumilia.
    Alisema kama ni kurejesha fedha zao, anayepaswa kufanya hivyo ni Twite mwenyewe na si klabu ya Yanga.
    Hanspope alisema wao waliingia mkataba na Twite kupitia klabu yake ya APR na Shirikisho la Soka la Rwanda, hivyo walipaswa kuomba hati ya uhamisho kutoka Rwanda na si Congo.
    "Haya mambo lazima ufike wakati yafikie mwisho. Haiwezekani klabu imesikia kwamba mchezaji amesajiliwa na klabu fulani na yenyewe inamfuata kuzungumza naye,"alisema.
    Hanspope alisema bado wanaamini kwamba Twite ni mchezaji wao na kama itatokea vinginevyo, watapambana hadi haki yao ipatikane.
    Yanga imemsajili Twite, wakati tayari akiwa amekwishaini Simba SC, baada ya kumrudisha kwenye uraia wake wa asili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), badala ya Rwanda aliopewa wakati akicheza nchini humo na kumbadili jina pia.
    Kwa kumbadili uraia, Yanga walipata na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji huyo, kutoka Shirikisho la Soka (DRC), na kuwaacha Simba wakihangaika bila mafanikio kupata ITC ya mchezaji huyo kutoka FERWAFA, Shirikisho la Soka la Rwanda. 
    Yanga inamsajili Twite kama mchezaji kutoka St Eloi Lupopo, klabu ambayo aliichezea kabla ya kutua APR mwaka 2006 kwa pamoja na ndugu yake, Kabange. Lakini mchezo uliochezwa hapa ni kwamba Twite alikuwa anacheza kwa mkopo APR.
    Habari zaidi zinasema, Yanga inamsajili pia na pacha wake Mbuyu (pacha wa kuzaliwa kabisa), Kabange, kwa sababu wachezaji hao kawaida yao kucheza timu moja daima.
    Huko nyuma, Yanga iliwahi kuifanyia tena Simba ‘umafia’ kama huu katika usajili wa wachezaji, Charles Boniface Mkwasa na Yussuf Ismail Bana, miaka ya 1980.
    Simba ilimsaiji beki wa Pamba kama Yussuf Bana, lakini Yanga wakaingilia kati na kumsajili kwa jina la Yussuf Ismail Bana, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa Shirikisho, TFF), wakati huo Said Hamad El Maamry akamuidhinisha beki huyo kucheza Yanga.
    Simba walijaribu kumuiba kiungo Charles Boniface, aliyesajiliwa Yanga kutoka Tumbaku ya Morogoro na kumsajili, lakini baadaye Yanga wakamsajili pia na kumbadili jina, wakimpa Charles Boniface Mkwasa.
    Mkwasa alifungiwa na FAT ya El Maamry kabla ya kufunguliwa baadaye na kuendelea kukipiga Yanga.
    Japokuwa kinachozungumzwa kwa sasa ni kwamba, mtoto wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ridhiwani Kikwete amewasaidia Yanga kumbadili njia Mbuyu, lakini uchunguzi wa kina uliofanywa na BIN ZUBEIRY umegundua mtoto huyo wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete hajahusika kabisa na usajili wa beki huyo, bali ni Bin Kleb.
    Kulingana na uzoefu wa ‘fitina za soka ya bongo’, inawezekana Simba wanamtaja Ridhiwani, ili ionekanane wamemkosa mchezaji huyo kwa nguvu za vigogo wa serikali, wakati ‘ubabaishaji’ wao wenyewe.
    Swali gumu ambalo bado litaendelea kuwaumiza wana Simba ni kwamba, akijua kwamba mchezaji huyo wakati anamsajili na Yanga pia walikuwa wanamfukuzia, kwa nini Rage alimuacha Rwanda, ambako Bin Kleb alibaki pia.
    Na hiyo inaumiza zaidi inapokumbukwa kwamba beki wao Kevin Yondan, alisaini na kujiunga na Yanga, wakati tayari akiwa amekwishasaini kuendelea kuichezea kla bu hiyo- maana yake viongozi wa Simba hawajifunzi kutoka na makosa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA KUMSHITAKI KIGEUGEU MBUYU TWITE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top