• HABARI MPYA

    Monday, August 27, 2012

    YANGA WAREJEA DAR BILA TWITE, SIMBA BADO WANA RB YAKE


    Na Mahmoud Zubeiry
    MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam wametua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam mida hii, wakitokea Rwanda walipokuwa kwa wiki moja kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki, ya mwisho jana wakishinda mabao 2-1 dhidi ya Polisi kwenye Uwanja wa Amahoro.
    Hata hivyo, Yanga imetua bila beki wake mpya, Mbuyu Twite iliyemsajili kutoka St Eloi Lupopo, ingawa alikuwa anachezea APR na Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa amesema kuna mambo anakamilisha na atatua Dar es Salaam ndani ya saa 48 kuanzia leo.
    “Na tuna imani Jumamosi katika mechi yetu na Coastal Union Uwanja wa Taifa atakuwepo kutambulishwa rasmi,”alisema Mwesigwa.
    Kuhusu mpango wa Simba SC, kumfungulia kesi Polisi na kumvizia akitua tu nchini imkamate kwa kuwatapeli dola za Kimarekani 30,000, Mwesigwa alisema; “Simba sio Polisi, na Yanga ni klabu ambayo inafanya mambo yake kwa utaratibu, kwa hivyo hatuna wasiwasi na hilo,”alisema.
    Kabla ya kusaini Yanga, inadaiwa Twite alisaini Simba na kupewa dola za Kimarekani 30,000 lakini baadaye akarudisha fedha hizo kupitia viongozi wa APR na Lupopo, ingawa Simba walikataa kuzipokea.
    Lakini tayari Simba SC wamesajili beki mwingine kutoka Kenya, Paschal Ochieng kama mbadala wa beki huyo wa kimataifa wa Rwanda- na sasa inachodai ni fedha zake.
    Yanga ilimaliza ziara yake jana nchini Rwanda kwa ushindi wa mabao 2-1, wafungaji Stefano Mwasyika aliyesawazishia, baada ya Fabrice kutangulia kuifungia Polisi na Nahodha Msaidizi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akafunga la pili.
    Katika mchezo wa awali Ijumaa, Yanga waliwachapa mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Amahoro mjini Kigali.
    Yanga ambao siku moja kabla ya mechi hiyo ya kwanza, walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame, siku hiyo mabao yake yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
    Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
    Yanga itaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara, inayotarajiwa kuanza Septemba 15 na Jumamosi itacheza na mabingwa wa Ligi Kuu 1988, Coastal Union.
    Yanga ilikwenda Rwanda na msafara wa watu 42, wakiwemo wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
    Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
    Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’, Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAREJEA DAR BILA TWITE, SIMBA BADO WANA RB YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top