![]() |
| Yanga baada ya kuwasili mjini Kigali, Rwanda. Picha zote na Saleh Ally, Mhariri kiongozi magazeti ya Championi. |
![]() |
| Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji baada ya kupokewa na Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, Milutin Sredojevic 'Micho' (kushoto) |
![]() |
| Manji kulia akijadiliana mambo na Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga |
![]() |
| Wachezaji wa Yanga mjini Kigali |
Na
Mahmoud Zubeiry
YANGA imefika salama mjini Kigali, Rwanda tayari kwa
kambi yao ya kujiandaa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
inayotarajiwa kuanza Septemba 15, mwaka huu.
Akizungumza kwa simu kutoka Kigali, Kocha Mkuu wa
Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet aliiambia BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, kwamba
kikosi kizima kipo tayari Kigali kwa kambi hiyo, lengo likiwa ni kurejesha
ubingwa wa Ligi Kuu Jangwani.
Kuhusu beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite
mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mtakatifu Tom alisema
atajiunga na timu Kigali. Kwa sasa, Mbuyu yupo nyumbani kwao kwa asili, DRC kwa
mapumziko mafupi kabla ya kuja kuanza maisha mapya Jangwani.
Kikosi kamili cha Yanga kilichopo Kigali ni; Makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed.
Mabeki; Shadrack Nsajigwa (Nahodha), Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar
Joshua, David Luhende na Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin
Yondan, Mbuyu Twite, Ibrahim Job na Ladislaus Mbogo.
Viungo; Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’ na Salum Telela, Nizar
Khalfan, Shamte Ally, Idrisa Rashid, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Rashid Gumbo
na Nurdin Bakari.
Washambuliaji; Said Bhanaunzi ‘Spider Man’, Hamisi Kiiza ‘Diego’, Didier
Kavambagu na Jerry Tegete.
Kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Simon Msuva, wanaendelea kukomazwa
katika kikosi cha kwanza, wakitokea kikosi cha pili. Awali Yanga ilikuwa icheze
na Coastal Union, lakini mechi hiyo imefutwa.
Akiwa anaingia mwezi wa pili tangu aanze kazi Yanga,
tayari Tom amekwishaweka Kombe moja kwenye kabati la mataji la Yanga, ambalo ni
la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili
mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga
Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na
Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo,
Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba
katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye
ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka
1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo,
Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said
Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa,
Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120,
Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo,
Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya
makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa
raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa
Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa
Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu
wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.






.png)
0 comments:
Post a Comment