• HABARI MPYA

    Wednesday, August 29, 2012

    SINA GARI NASHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YANGU IPASAVYO YANGA- MTAKATIFU TOM

    . Asema hakuwa kumtaka Mrisho Ngassa Jangwani
    . Ikitokea timu Tanzania kumpandia dau...
    . Akoshwa na vitu vya dogo Simon Msuva, asema...

    Na Mahmoud Zubeiry
    BIN ZUBEIRY inakuletea mahojiano ya maswali na majibu na Kocha Mkuu wa mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintfiet 'Mtakatifu Tom' kuhusu masuala mbalimbali katika klabu yake. Endelea.
    Mtakatifu Tom kushoto, akiwa na BIN ZUBEIRY

    BIN ZUBEIRY: Habari za leo kocha?
    SAINTFIET: Nzuri, habari na wewe

    BIN ZUBEIRY: Salama. Vipi unaendeleaje na kazi?
    SAINTFIET: Vizuri

    BIN ZUBEIRY: Vipi kuhusu timu kwa ujumla?
    SAINTFIET: Timu yangu iko vizuri, isipokuwa wachezaji wachache ni wagonjwa. Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Juma Seif, Idrisa Assenga na Athumani Iddi.
      
    BIN ZUBEIRY: Wanasumbuliwa na nini?
    SAINTFIET: Wengine Malaria, wengine mafua

    BIN ZUBEIRY: Sawa pole sana, hawajafanya mazoezi tangu lini?
    SAINTFIET: Wengine tangu Jumamosi, wengine walicheza Jumapili, lakini hakuna aliyefanya mazoezi kabisa kati yao

    BIN ZUBEIRY: Sawa, nafikiri Simon Msuva ameleta changamoto mpya kwako katika upangaji wa kikosi cha kwanza (safu ya ushambuliaji)
    SAINTFIET: Ndio, ananifurahisha sana

    BIN ZUBEIRY: sahihi, bado unajuta kumkosa Mrisho Ngassa?
    SAINTFIET: Sijawahi kujuta chochote, Ngassa ni mchezaji mzuri, lakini anachezea Simba, hivyo hanihusu na siwezi kumzungumzia.

    BIN ZUBEIRY: Lakini alikuwa mbioni kujiunga na timu yako
    SAINTFIET: Sikuwahi kuhusishwa katika uhamisho wake, hakuna yeyote aliyenifuata kuomba maoni yangu wala ushauri
    Mtakatifu Tom na vijana wake

    BIN ZUBEIRY: Ukiwa na Frank Domayo na Athumani Iddi ‘Chuji’ katika nafasi moja, upi mpango wako katika kikosi cha kwanza?
    SAINTFIET: Hilo siwezi kuongea kwenye vyombo vya habari sababu wote ni wachezaji wangu. Na pia inategemea na mechi na mechi.

    BIN ZUBEIRY: Baada ya miezi miwili ya kuwa na Yanga, unaweza kusema nini kuhusu klabu hiyo?
    SAINTFIET: Ninafurahia sana ushirikiano kutoka kwa wachezaji wangu na benchi la ufundi kwa ujumla pamoja na viongozi

    BIN ZUBEIRY: Ikitokea klabu nyingine hapa nchini ikakupa ofa ya mshahara mzuri zaidi unaopewa Yanga, utakubalia kuhamia huko?
    SAINTFIET: Haa haa, swali zuri sana, ina maana nihame Yanga nikipata ofa yoyote?

    BIN ZUBEIRY: Ndio, kutoka klabu yoyote nchini
    SAINTFIET: Sijawahi kusikia klabu yeyote inanitaka

    BIN ZUBEIRY: Ikitokea…
    SAINTFIET: Siwezi kuzungumzia mambo ambayo hayajatokea, kwa sababu inategemea na hali halisi itakavyokuwa katika klabu yangu ya sasa wakati itakapotokea hiyo ofa

    BIN ZUBEIRY: Nini mipango yako ya muda mrefu katika timu?
    SAINTFIET: Nipo hapa kwa ajili ya kushinda ubingwa. Nachukia kufungwa. Nimecheza mechi 12 tangu nifike hapa, nimeshinda 11. Tangu mwaka 2008, nimefungwa mechi sita tu, hivyo nataka kushinda popote ninapofanya kazi yangu ya ukocha

    BIN ZUBEIRY: Unahusika kwa namna yoyote katika timu ya vijana ya Yanga?
    SAINTFIET: Ndio, kwa nini unauliza?
    U20 ya Yanga mazoezini Kaunda

    BIN ZUBEIRY:  Nataka kujua
    SAINTFIET: Nataka kuhusika kikamilifu, kutokana na ukweli kwamba bado sijapewa gari, siwezi kutekeleza hilo jukumu ipasavyo kwa sasa.

    BIN ZUBEIRY: Makocha wengi hata hapa Tanzania, mwishoni mwa msimu hupandisha wachezaji kutoka timu zao za vijana, vipi wewe?
    SAINTFIET: Tunao Simon Msuva, Omega Seme, Frank Damayo, wote ni wachezaji wa timu ya vijana…

    BIN ZUBEIRY: Lakini wote wametoka timu nyingine na kusajiliwa Yanga, tena kwa fedha nyingi.
    SAINTFIET: Mradi wa maendeleo ya vijana siyo U20 , maendeleo ya vijana ni kuanzia U8, U10, U12, U14, U16 na U18!

    BIN ZUBEIRY:  Tutarajie hilo siku moja katika Yanga chini ya utawala wako?
    SAINTFIET: Ningepeda pia, hilo lilikuwa moja ya maombi yangu kwa viongozi, nataka kujenga akademi kama ya ASEC Mimosas. Nilikuwa Mkurugenzi wa Ufundi Nigeria na klabu ya kulipwa Uholanzi. Nimewahi kuandika miradi ya maendeleo na ninajua vema namna ya kuendesha akademi.
    Ubingwa wa Kagame, matunda ya Mtakatifu Tom Jangwani

    BIN ZUBEIRY: Tatizo nini kwa sasa katika klabu yako, Yanga?
    SAINTFIET: Oh, tunatakia kuanzia kwenye sifuri, tunahitaji malazi (kwa wachezaji), kocha na huduma nyingine za muhimu kwa vijana.

    BIN ZUBEIRY: Huo ni mpango wako haswa katika Yanga?
    SAINTFIET: Ndio, kama klabu ikinipa sapoti katika hili. Nafikiri ni muhimu sana kwa Yanga na soka ya Tanzania kwa ujumla, tunahitaji kuwa na akademi nzuri haswa.
    Yanga katika Kombe la Kagame; Hapa ilikuwa ni Robo Fainali na Mafunzo wakati wa mikwaju ya penalti

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SINA GARI NASHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YANGU IPASAVYO YANGA- MTAKATIFU TOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top