• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 28, 2012

  KIPA MPYA SIMBA AFURAHIA KUCHOTA UJUZI KWA KASEJA

  Hamadi Waziri

  Na Prince Akbar
  HAMADI Waziri, mmoja wa makipa wa akiba wa Simba, amesema anafurahi kuwa katika timu hiyo pamoja na kipa bora kabisa nchini, Juma Kaseja kwani anajifunza mambo mengi kutoka kwa Tanzania One huyo.
  Akizungumza mjini Arusha, juzi baada ya mechi dhidi ya Mathare United ya Kenya, Hamadi aliyesajiliwa kutoka JKT Oljoro alisema kwamba Kaseja ni kipa mwenye uwezo wa hali ya juu na kuwa naye pamoja ananufaika mno kwa kujifunza mambo mengi kutoka kwa kipa huyo.
  “Kaseja pamoja na kuwa na Nahodha wetu, pia ni kaka yetu ambaye anatuongoza vizuri, kwa kweli binafsi nafurahia sana fursa hii,”alisema.
  Lakini pia kipa huyo chipukizi aliyeonyesha uwezo mkubwa kwa siku chache za kuwa na klabu huyo, alisema pia anafurahi mno kuwa chini ya kocha maalum kwa makipa, James Kisaka ambaye anawafundisha vizuri.
  “Niseme tu mimi sijawahi kuwa chini ya kocha wa makipa ambaye anafundisha vizuri kama kocha Kisaka, naamini kabisa hii ni fursa nzuri kwangu kukuza uwezo wangu ili siku moja nitimize ndoto zangu za kuwa kipa bora nchini,”alisema Waziri.
  Makipa wote wa akiba wa Simba, Waziri na Albert Mweta juzi walionyesha viwango vizuri katika mchezo wa kirafiki wa klabu hiyo dhidi ya Mathare United ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
  Mweta aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Toto African ya Mwanza juzi alianza na kumaliza dakika 45 bila kufungwa, kabla ya kufungwa bao moja kipindi cha pili, tena baada ya mabeki Paschal Ochieng na Juma Nyosso kuchanganyana.
  Akiwa langoni, Mweta aliokoa hatari kadhaa na kuonyesha kwamba ni kipa aliye tayari hata mechi kubwa na alipoingia Hamadi naye pia alionyesha kiwango kizuri na kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
  Makipa hao, walidaka jana kwa sababu kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja alikuwa mgonjwa. Katika mchezo huo, bao la penalti dakika ya 81 lililofungwa na kiungo Kiggi Makassy, lilitosha kuipa Simba ushindi wa mabao 2-1, kabla ya kuingia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam.
  Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka Ghana, Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir Maftah.  
  Mathare walisawazisha bao hilo dakika ya 68, mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome ya Simba SC, iliyokuwa ikiogozwa na Paschal Ochieng na Juma Nyosso.
  Beki wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari, Uhuru Suleiman dakika ya 80 na ushei na refa akaamuru ipigwe penalti, iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa guu la kushoto la Kiggi Makassy.
  Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, Haruna Moshi ‘Boban’ akirudishwa katika nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa washambuliaji halisi. Alicheza kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata kuwapokonya mipira viungo wa timu pinzani.
  Dakika za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira kwa nguvu miguuni mwa mshambuliaji wa Mathare, baada ya Maftah kupitwa, kuashiria kwamba kijana amebadilika si yule wa kukaba kwa macho.
  Felix Sunzu na Akuffo walikuwa wanapishana vizuri pale mbele na waliitia misukosuko ngome ya Mathare- zaidi ni kwamba wawili hawa wanahitaji muda zaidi wa kucheza pamoja ili kutengeneza safu kali ya ushambuliaji ya Simba SC.
  Juma Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa mechi hiyo kwa sababu walikuwa wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya kuumia. 
  Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
  Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
  Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 
  Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Wilbert Mweta/Hassan Waziri, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Paul Ngalema, Paschal Ochieng, Komabil Keita/Juma Nyosso, Salum Kinje/Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto/Haruna Shamte, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Abdallah Juma/Amri Kiemba na Daniel Akuffo/Uhuru Suleiman.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA MPYA SIMBA AFURAHIA KUCHOTA UJUZI KWA KASEJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top