• HABARI MPYA

    Thursday, August 23, 2012

    KOCHA MPYA AZAM ALETA MFUMO WA KUTISHA, SIMBA WAJIPANGE

    Azam FC

    Na Mahmoud Zubeiry
    MFUMO mpya wa uchezaji wa Azam FC, chini ya kocha wake mpya, kutoka Serbia, Boris Bunjak ni wa kushambulia kwa haraka na mfululizo, bila kumpa mpinzani nafasi ya kupumua, ambao unahitaji wachezaji walio fiti kwa angalau asilimia 70 ili kuumudu vyema.
    Kwa kujua hilo, kocha Bunjak amekuwa akiwafua vikali wachezaji wa timu hiyo katika mazoezi yanayoendelea Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ili wawe fiti kiasi cha kuumudu mfumo huo wa kucheza na mabeki wane sawa na viungo na washambuliaji wawili.
    Kulingana na mazoezi ya Bunjak Azam, hataki mabeki wachezee mpira nyuma na zaidi anataka mashambulizi ya kupitia pembeni, krosi kwa wingi au kwa ujumla mashambulizi ya moja kwa moja na mfululizo.
    Ni matarajio, iwapo Azam wataumudu vema mfumo huo na kulingana na aina ya wachezaji iliyonao, wengi wenye kasi na wepesi, dhahiri timu hiyo iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita katika Ligi Kuu, itakuwa tishio msimu ujao.
    Bunjak alirithi nafasi ya Muingereza, Stewart Halla ambaye alifukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga mwezi uliopita.
    Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
    Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
    Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
    Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
    Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
    Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
    Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.
    Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.  
    Bunjak anatarajiwa kuiongoza Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inatarajiwa kuchezwa Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya bingwa wa ligi hiyo, Simba SC.
    Habari za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema kwamba, kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema wa mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.
    Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano yanayoendelea.
    Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita uliridhia kuanzia msimu ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na klabu za Ligi Kuu mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana na kuhusisha pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.
    Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya mkataba mpya wa udhamini na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa Septemba 8, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka         Mshindi       Matokeo
    2001             Yanga           2-1 Simba
    2010             Yanga           0-0 Simba (3-1penalti)
    2011             Simba           2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MPYA AZAM ALETA MFUMO WA KUTISHA, SIMBA WAJIPANGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top