MWENYEKITI wa Simba SC, jana amekaririwa na vyombo vya
habari nchini akimshutumu mtoto wa kigogo kimoja nchini kumshinikiza Rais wa
APR ya Rwanda, Meja Alex Kagame ampeleke Yanga, beki Mbuyu Twite, wakati
alikuwa amekwishasaini Simba na kupewa fedha.
Na Mahmoud Zubeiry |
Rage amelalamika sana na akapiga hatua kubwa zaidi, akaanza
kuwakashifu viongozi wa Yanga, wana fedha chafu za EPA.
Yote haya yanakuja baada ya kuzidiwa kete katika kuwania
saini ya Twite. Namfahamu Rage na hii ndio desturi yake. Anapopandisha jazba
huweza kusema lolote, bila ya kujali chochote.
Kabla ya kuzungumzia sakata la mchezaji huyo, nianze kwa
kumuelewesha tu Rage, asitazame boriti kwenye jicho la wapinzani wake, Yanga
akasahau kibanzi kilichopo kwenye jicho lake.
Rage anafahamu fika, mambo ambayo yako mahakamani huwa
hayajadiliwi nje ya Mahakama na hakuna asiyefahamu kwamba suala la wizi wa
fedha kwenye Akaundi ya Madeni ya Nje (EPA), lilifikishwa mahakamani na baadhi
ya waliokutwa na hatia, hivi sasa wanatumikia kifungo jela.
Na hivi karibuni, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na Wahariri wa vyombo vya Habari nchini, Ikulu
mjini Dar es Salaam, amerudia kusema juu ya hilo, kwamba serikali haimlindi
yeyote na ilizikabidhi mamlaka husika zichukulie hatua hilo na kwa kuwa mamlaka
hizo ni huru, hawawezi kuziingilia.
Sasa inakuwa jambo la ajabu, Rage anapothubutu kumuhukumu
mtu mwingine nje ya Mahakama juu ya EPA.
Ni sawa tu na leo hii, atokee mtu aanze kumzungumzia yeye
kuhusu dola 40,000 za Yanga za mwaka 1998 alizochukua CAF (Shirikisho la Soka
Afrika) au tuhuma nyingine lukuki za ubadhirifu wa mali za Chama cha Soka
Tanzania (FAT, sasa Shirikisho, TFF), atakuwa hamtendei haki, kwa sababu Mahakama
ilikwishaamua.
Awali, Rage alihukumiwa kifungo jela, kabla ya kutoka kwa msamaha
wa Rais, baadaye akaenda Mahakama ya Rufaa, kukata rufaa kupinga hukumu hiyo,
akafanikiwa, mahakama ikamsafisha na ndio maana leo ni Mbunge na Mwenyekiti was
Simba, vinginevyo asingeweza kupata haki ya kugombea hata Ukatibu Kata.
Naomba niwaombe radhi wasomaji wangu na Rage pia, kwa
kukumbushia suala la dola 40,000 na kifungo cha Rage kabla ya kutoka kwa
msamaha wa Rais, kwa kuwa natambua si busara kuzungumzia mambo ambayo
yamefikishwa Mahakamani.
MTOTO WA KIGOGO;
Hajamtaja jina, lakini dhahiri hapa anazungumziwa Ridhiwani,
mtoto wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Nani asiyejua kama Ridhiwani ni Yanga na
Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga na sidhani kuna dhambi katika hilo, ikiwa
Waziri Mkuu wa zamani, ‘Simba wa Vita’, Mzee Rashid Mfaume Kawawa alikuwa
Simba.
Simba na Yanga ni timu za Watanzania, na ndio maana Profesa
Juma Athumani Kapuya, Rage mwenyewe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
Zitto Kabwe, Iddi Azzan na wengine miongoni mwa vigogo wa nchi yetu ni Simba.
Kama Ridhiwani alijaribu kuisaidia Yanga, timu yake kuna
dhambi gani, ikiwa mwaka 2005 Kapuya aliisaidia timu yake, Simba SC kutompoteza
beki Victor Costa, ingawa alikuwa amesaini Yanga na kupewa fedha?
Mimi namheshimu rais wetu, Kikwete na sidhani kama ana muda
wa kushughulika na ‘upuuzi’ wa Simba na Yanga- lakini kama mzazi pia ambaye
anatambua Ridhiwani kijana wake naye ni baba wa familia pia, ana uhuru wake
katika mambo yake. Hawezi kumuingilia.
Yanga imepitia wakati mgumu na Kikwete yupo pale pale Ikulu
na hajaonyesha hata dalili za kutaka kuwasaidia Yanga. Kikwete akiwa Ikulu,
alileta kocha kwa ajili ya timu ya taifa, turudi enzi zile Rage na Samuel Sitta
wakiwa CDA, walilitumia shirika hilo kwa manufaa ya timu ya taifa au Simba?
Watu wanakumbuka haya mambo ndio maana namtahadharisha Rage, asiangalie boriti
kwenye jicho la wapinzani, wakati jicho lake lina kibanzi.
Mambo ya kuchafuana si mazuri na yamepitwa na wakati- Rage
kama ameamua kuwa Mwenyekiti was Simba, basi apambane na changamoto zote bila
ya kumnyooshea mtu kidole na kwa kweli umefika wakati Rage aachane na ‘Saisa za
Majitaka’, kwanza hata umri wake tu haumruhusu tena kufanya mambo kama hayo,
amekwishakuwa mtu mzima sasa.
Huyo Ridhiwani kama ndio staili yake hiyo kutisha watu, kwa
nini asianzie hapa nyumbani kuwatisha viongozi wa Azam katika suala la Mrisho
Ngassa wampeleke Yanga? Rage amewahi kupewa onyo kali na TFF kwa kosa la kutoa
kauli za uchochezi na ajabu hajaacha, kwani kauli zake dhidi ya mtoto wa kigogo
ni za uchochezi. Ni za hatari.
SAKATA LA MBUYU TWITE
Kama kuna mtu wa kwanza wa kulaumu juu ya Simba kumpoteza
Mbuyu Twite, basi ni Aden Rage. Kwa nini? Alipofika Kigali, baada ya kumpa fedha
beki huyo na kumsainisha mkataba, alijua fika na Yanga nao wanamfuatilia
mchezaji huyo.
Yanga wale wale, waliomchukua Kevin Yondan na kumsainisha
mkataba, wakati tayari amesaini mkataba (kwa mujibu wa Simba) wa kuendelea
kuichezea klabu yake, Simba SC.
Ajabu Rage akijua kabisa, Yanga si waungwana, akamuacha
Twite Kigali, yeye akawahi Mkutano Mkuu na baadaye shughuli za Bunge, huku
nyuma Yanga wakafanya ambacho kinamsababisha leo yeye azungumze huku mapovu
yanamtoka mdomoni.
Rage alitakiwa arudi Dar es Salaam na Mbuyu Twite, apokewe
na maelfu ya wana Simba halafu tungeona kama angethubutu kusaini Yanga. Rage
pamoja na uzoefu wake wote katika masuala ya usajili na fitina za mpira, hapa
alichemka na badala ya kutafuta mchawi, ni vema akajilaumu mwenyewe.
Nimependa alivyomalizia mazungumzo yake jana, alisema wao
watatafuta mchezaji mwingine mzuri na anachoomba tu, Simba warudishiwe fedha
zao, kiasi cha dola 40,000 hivi, pamoja na gharama za nauli, kwake, mchezaji
mwenyewe na mawakili waliotayarisha mkataba aliosaini Twite. Safi.
TUACHE UHUNI KATIKA SOKA YETU:
Soka yetu imegubikwa na mambo ya kihuni, ambayo wenyewe wanayaita
ya kimjini, ambayo siku zote mimi tangu nipo DIMBA, kuanzia Mwandishi hadi
Mhariri, nilikuwa nayapinga vikali, kwa sababu najua athari zake ni kuididimiza
soka yetu.
Leo Simba wakilia kuhusu Twite, Yanga watawaambia;
Mnakumbuka Costa? Na bado historia inaanzia mbali tangu ya 1960, Simba na Yanga
zilikuwa zinapokonyana wachezaji.
Ila katika dunia ya leo, inayotawaliwa na utaalamu,
taratibu, kanuni na sheria, kwa nini tuendelee kuyalea mambo kama haya?
Siyo tu sijapendezewa na staili waliyoitumia Yanga kumsajili
Twite, lakini pia sijapenda staili waliyotumia Simba kumsajili Ramadhan Chombo
‘Redondo’, ambayo leo inawaliza Azam.
Huo ni upande mmoja, upande wa pili, kuhonga wachezaji wa
timu pinzani na marefa- hili pia silipendi na ni sehemu ya uhuni, ambao unapoteza
maana halisi ya soka ambayo FIFA wanaitaka. Soka ya kiungwana. Hayo yalikuwa
mapitio tu, leo ujumbe wangu ulikuwa Mh. Alhaj Rage; asikumuke EPA tu, kuna
dola 40,000 za Yanga, je watu wakumbushie hizi? Nawatakia saumu njema na kwa
ujumla mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan inshaallah.
0 comments:
Post a Comment