• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 27, 2012

  MANJI ATUMBUKIZA FEDHA KAGAME  Manji
  Na Prince Akbar 
  KAMPUNI ya Quality Group Limited, imeongeza dola za Kimarekani 20,000 zaidi ya Sh. Milioni 30 za Tanzania kwenye zawadi za michuano ya soka ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality, Yussuf Manji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, alimpa ahadi hiyo rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati klabu hiyo ilipomtembelea rais huyo Ikulu ya Rwanda, Alhamisi kijiji cha Urugwiro.
  Kwa dola hizo 20,000 sasa kitita cha zawadi za washindi wa michuano hiyo kinatuna hadi kufika dola 80,000 kufuatia dola 60,000 zinazotolewa na rais Kagame.
  Mwaka 2002, rais Kagame aliweka rekodi ya kuwa mdhamini wa kwanza kutoa zawadi za mashindani hayo, dola 60,000 ambazo zimekuwa zikigawanywa kwa washindi watatu wa juu.
  Mbali na zawadi hizo, rais Kagame pia anatoa dola 15,000 kila mwaka kwa maandalizi ya michuano hiyo na kufanya mchango wake jumla kuwa dola 75,000.
  Kwa mchango wake huo mkubwa, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeyapa jina la rais huyo mashindano hayo.
  Mwakani, michuano ya CECAFA Kagame itafanyika mjini Kigali kuanzia Januari, kwa mujibu wa Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye.
  Musonye ataenda Kigali mapema mwezi ujao kukutana na viongozi wa Wizara ya Michezo kujadili zaidi kuhusu maandalizi ya michuano hiyo.
  Yanga ni mabingwa wa Kombe kwa miaka mfululizo, katika fainali mbili mfululizo zilizofanyika Dar es Salaam hivyo kufanya wawe wametwaa Kombe hilo mara tano jumla na mwakani wataongozana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC kwenye michuano hiyo.
  Wenyeji Rwanda wanatarajiwa kuwakilishwa na mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, APR, ambao mwaka huu waliambulia nafasi ya nne baada ya kufungwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na Polisi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANJI ATUMBUKIZA FEDHA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top