• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 27, 2012

  COASTAL YASHINDA MKWAKWANI, LAKINI...

  Coastal Union

  Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
  COASTAL Union imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Bao pekee la mabingwa hao wa 1988, lilitiwa kimiani na beki mpya aliyesajiliwa kutoka Simba SC, Juma Jabu dakika ya 32 baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi akiteleza kutokea wingi ya kushoto.
  Katika mchezo huo, Suleiman Kassim 'Selembe' alikosa penalti dakika ya 26, baada ya Aziz Gilla kuangushwa kwenye eneo la hatari na refa Ibrahim Kidiwa kuamuru adhabu hiyo, lakini kipa wa Oljoro alipangua na pamoja na kiungo huyo Mzanzibar kuuwahi mpira kuupiga tena, lakini kipa huyo akaokoa tena
  Huo ni ushindi wa kwanza wa Wagosi hao wa Kaya, ndani ya mechi tatu zsa kujipima nguvu, ikitoka kufungwa 3-2 na Bandari mjini Mombasa, Kenya na 1-0 dhidi ya Polisi mjini Morogoro.
  Pamoja na ushindi huo, mashabiki wa Coastal hawakuridhishwa na kiwango cha timu na kuanza kubeza uwezo wa makocha wa timu hiyo, Juma Mgunda na msaidizi wake, Habib Kondo.
  Habari za ndani zinasema kwamba Coastal inafikiria kubadilisha benchi la ufundi kutokana na kutoridhishwa na uwezo wa timu.    
  Coastal iliwekeza kwenye usajili wa kishindo, ikiamini itafanya vizuri katika Ligi Kuu, lakini kwa matokeo haya ya awali tayari hofu imeanza kuingia na wakati mashabiki wakitilia hofu uwezo wa makocha, wengine wanatilia hofu uwezo wa wachezaji waliosajiliwa, wakiamini inaweza kuwa ni bora kwa majina tu.
  Kikosi cha Coastal kinaundwa na makipa; Juma Mpongo, Abraham Chove na Rajab Kaumba, mabeki; Said Sued (Nahodha) Mbwana Kibacha (Nahodha Msaidizi) Othman Omary, Juma Jabu, Ismail Suma, Jamal Machelenga, Cyprian Lukindo na Philipp Mugenzi.
  Viungo watakuwa ni Jerry Santo, Razack Khalfan, Mohamed Binslum, Khamis Shango, Mohamed Issa, Mohamed Soud, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Lameck Dayton, Joseph Mahundi, Aziz Gilla na Shaffih Kaluani, wakati washambuliaji ni Nsa Job, Atupele Green, Danny Lianga na Pius Kisambale.
  Mbali na Kocha Mkuu, mshambuliaji wake wa zamani, Mgunda,  na Msaidizi wake, beki wa zamani wa Pan African, Habibu Kondo, benchi la ufundi la Coastal linakamilishwa na kocha wa viungo, mchezaji wake wa zamani, Ally Jangalu na kocha wa makipa Bakari Shime.
  Wagosi hao wa Kaya watakuwa na mechi mbili mfululizo mwishoni mwa wiki hii mjini Dar es Salaam, Jumamosi wakianza na Yanga na Jumapili na Simba SC Uwanja wa Taifa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: COASTAL YASHINDA MKWAKWANI, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top